Habari

Kidero na wengine waondolewa kesi ya kuiba Sh213M

Na SAM KIPLAGAT November 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Evans Kidero Novemba 6, 2025 aliondolewa mashtaka kwenye kesi ya wizi wa Sh213 milioni ambazo zilidaiwa kupotea katika kaunti wakati wa utawala wake.

Mahakama ilimwaachilia Bw Kidero, aliyekuwa katibu wa kaunti Lilian Ndegwa, aliyekuwa afisa mkuu wa fedha Mutuku Kiamba na aliyekuwa waziri wa fedha na mipango Gregory Mwakanongo.

Wengine ambao waliondolewa mashtaka ni aliyekuwa kaimu afisa mkuu wa fedha Luke Mugo na kaimu mkuu wa hazina ya fedha Maurice Ochieng’ Okere.

Wote hao hao ilibainika hawakuwa na kesi ya kujibu.

Kesi hiyo imechukua miaka mitano ikisikizwa kabla ya uamuzi kutolewa.Mashtaka dhidi yao yalidai kuwa walipanga njama kuibia kaunti hali ambayo ilichangia kupotea kwa Sh213 milioni.

Pesa hizo zilipotea kati ya Januari 16,2014 hadi Januari 25. 2016.

Mashtaka mengine yalishirikisha njama ya kushiriki ufisadi, kutumia afisi vibaya, kutwaa mali kinyume cha sheria na kukosa kulipa ushuru. Mahakama ilisema kuwa maafisa hao wa kaunti hawakuwa na kesi ya kujibu na ikawaachilia kwa kufuata sheria.

Bw Kidero alidaiwa kupokea Sh24 milioni kutoka kwa Kampuni ya Lodwar.

Mashtaka yalionyesha kuwa alipokea Sh14 milioni kutoka kwa kampuni hiyo kuanzia Agosti 24, 2014 na Sh10 milioni zaidi kutoka kwa kampuni hiyo mnamo Septemba 11, 2014.

Wafanyabiashara John Githua na Grace Njeri wa kampuni hiyo nao walilaumiwa kwa kupokea pesa kutoka kwa kaunti bila kutoa huduma zozote.

Pia aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Uhasibu Stephen Ogago Osiro alilazimika kujitetea ikidaiwa alipokea mamilioni ya pesa kutoka kwa wafanyabiashara hao wawili.

Bw Kidero alikosoa kiongozi wa mashtaka akisema hakuwasilisha ushahidi kuhusu makubaliano kati yake na mshukiwa yeyote kuhusu ufisadi aliodaiwa kutekeleza.

Kwake makubaliano kati yake na anaodaiwa kushirikiana nao kuilaghai kaunti yalikuwa muhimu lakini hakuna jaribu au juhudi zozote zilifanywa na kuwasilisha makubaliano kama hayo kortini.

Bw Kiamba naye alisema alitekeleza majukumu yake bila kushirikiana na mtu yeyote kuibia kaunti.

Aliongeza kuwa shahidi wa upande wa kiongozi wa mashtaka aliidhinisha stakabadhi zote za malipo alizowasilisha kama ushahidi.“Ni uamuzi wangu kuwa upande wa mashtaka haujatoa ushahidi wowote kuonyesha Kidero alitumia mamlaka na afisi yake kujitajirisha kifedha,” akasema.