Avurugwa na ndoa ya zamani
MFANYABIASHARA ameshtakiwa kwa kuiba mali ambayo thamani yake ni Sh933,000 katika mtaa wa kifahari wa Karen, kaunti ya Nairobi.
Mary Waithera Gikonyo aliyeshtakiwa mbele ya hakimu mkazi mahakama ya Kibera. Agnetta Ogonda alieleza korti kupitia wakili wake John Swaka kwamba kesi hiyo inatokana na mzozo kati yake na mumewe waliyetengana.
Waithera aliyekabiliwa na mashtaka mawili aliyakanusha na kuomba mahakama imwachilie kwa dhamana.
“Hii kesi inatokana na mzozo wa kijamii ambapo mshtakiwa ametengana na mume wake wa zamani,” Bw Swaka alimweleza hakimu.
Wakili huyo alieleza mahakama makazi ambayo mshtakiwa anadaiwa amevunja lango kuu na madirisha na kusababisha hasara ya Sh335,000 ni nyumba yake.
“Wakati ukiwadia nitwasilisha ushahidi kuthibitisha nyumba anayodaiwa kuvunja na kuiba ni yake,’ Bw Swaka alimweleza hakimu.
Kesi hiyo ya kung’ang’ania mali inasikizwa na Mahakama kuu Milimani Nairobi.
Waithera alikana mashtaka mawili ya kuharibu mali na kuiba.
Alikana aliharibu nyumba ya Eric Munene na kuiba vifaa kadhaa ikiwamo ya dhahabu.
Waithera alikana alitekeleza wizi huo mnamo Machi 22,2025.
Nyumba anayaodaiwa kuharibu iko kwenye barabara ya Kumbe Road eneo la Hardy mtaani Karen.
Mtaa wa Karen uko katika eneo la uwakilishi bungeni la Lang’ata.
Mahakama ilielelezwa mshtakiwa alivunja lango kuu la makazi hayo ya Munene na kuharibu kamera ya CCTV, madirisha na mlango ambazo thamani yake ni Sh325,000.
Shtaka la pili ni wizi kinyume cha sheria nambari 268 na 275 za jinai.
Upande wa mashtaka umeeleza mahakama mshtakiwa aliiba saa ya dhahabu, Iphone, Kamera ya Video ya Samsung, tarakilishi tatu na saa mbili za ukutani.
Thamani ya bidhaa hizi ni Sh933,500.
Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 pesa tasilimu baada ya kusema upande wa mashtaka haujawasilisha ushahidi wowote kuthibitisha mshtakiwa atavuruga mashahidi.