Wabunge wapinga kupunguzwa kwa pesa za barabara za maeneobunge
WABUNGE wamepinga uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa kupunguza mgao wa fedha kwa kila moja ya maeneobunge 290 kwa Sh10 milioni, hatua ambayo serikali inasema inalenga kupata fedha za kuwalipa wanakandarasi wa miradi ya ujenzi wa barabara kote nchini.
Kupitia pendekezo lililoidhinishwa na Baraza la Mawaziri chini ya kifungu cha 6 (2)(c) na 32A cha Sheria ya Bodi ya Barabara ya Kenya, serikali inataka Bunge la Kitaifa kuidhinisha Sh5 kwa kila lita ya mafuta inayotozwa katika Hazina ya Ukarabati wa Barabara (RMLF), kwa lengo la kukusanya Sh120 bilioni katika kipindi cha miaka miwili kusaidia kulipa wakandarasi.
Katika mwaka wa fedha unaoendelea, kila eneobunge lilitengewa Sh63 milioni kupitia Mamlaka ya Barabara za Maeneo ya Mashambani (KeRRA) kwa ukarabati wa barabara za maeneobunge.
Waziri wa Barabara na Uchukuzi Bw Davis Chirchir aliwaambia wanachama wa Kamati ya Uchukuzi na Miundombinu kwamba iwapo pendekezo hilo litapitishwa na bunge, kila eneobunge litapokea Sh53 milioni badala ya Sh63 milioni.
Hata hivyo, mbunge wa Laikipia Mashariki, Bw Mwangi Kiunjuri, alitilia shaka mpango huo akiuliza, “Je, inawezekana kwa wabunge kukubali kupunguzwa kwa mgao huu?”
Aliongeza: “Tunapoteza kilomita nyingi za barabara za maeneobunge kwa sababu ya miradi mipya. Hii si haki kwa wananchi wetu.”
Kufikia Desemba 31, 2024, serikali ilikuwa na mikataba ya ujenzi wa barabara ya thamani ya Sh700 bilioni, ikiwa ni miradi ambayo haijakamilika pamoja na huduma zinazohusiana na miradi hii, ikiwemo fidia ya ardhi.
Mbali na suala hilo, kulikuwa na madeni ya Sh172 bilioni ya kazi zilizokamilika na kuthibitishwa, ambayo bado hayajalipwa.
Kwa mujibu wa Bw Chirchir, hali hiyo imesababishwa na upungufu wa bajeti kwa miaka kadhaa, hali iliyosababisha mirundiko ya madeni na wakandarasi wengi kuacha kazi kabla ya kukamilika.
Bw Kiunjuri aliwakumbusha maafisa wa wizara kuwa barabara nyingi zimeharibiwa na mvua kubwa na zinahitaji ukarabati wa dharura.
“Kupitia kwa pendekezo hili la Baraza la Mawaziri, huenda tusipate fedha za kutengeneza barabara katika maeneobunge. Tulitarajia kuongezwa kwa mgao, si kupunguzwa,” alisema kwa hasira.