Ashtakiwa kuwapora mayatima mali ya Sh25M
MKURUGENZI wa kampuni moja amefikishwa kortini kwa kuwaibia mayatima na mjane mali ya thamani ya Sh25milioni.
Tom Waiharo Njoroge , mkurugenzi wa Mass Labs Limited (MAL) alikabiliwa na mashtaka ya kuibia familia ya marehemu Joseph Santet Ole Shoona mali yake katika kipindi cha miaka minne.
Njoroge alikana kuibia familia ya marehemu mali kati ya Aprili 2021 na Oktoba 29 2025.
Njoroge alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina.
Alifunguliwa mashtaka matano na afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (ODPP).
Alidaiwa alivuruga mali ya mfu, kutengeneza stakabadhi feki,kughushi makubaliano ya kampuni ya MAL, kuwasilisha hati feki kwa afisi ya msajili iliyoko katika afisi ya mwanasheria mkuu.
Njoroge alishtakiwa kukaidi sheria za urithi nambari 45(1) na 45(2).
Njoroge alishtakiwa kuwa kati ya Aprili 2021 na Oktoba 29,2025 katika afisi za MAL zilizoko uwanja wa maonyesho ya kilimo (ASK) eneo la Jamuhuri alihamisha mali za MAL na kuziandikisha chini ya Apex Projects Limited.
Njoroge alikuwa mkurugenzi mwenza na Joseph Santet Ole Shoona (marehemu).
Hakimu alifahamishwa Njoroge alijiandikia mali za marehemu bila idhini ya Lawrence Lein Shoona, Caroline Lipaso Shoona na Lois Shena Shoona, ambao ni wasimamizi wa mali ya marehemu.
Mamo Desemba 6 2023 mshtakiwa alikana alitengeneza taarifa feki za makubaliano ya kuhamisha mali za MAL hadi kwa Apex.
Hakimu aliambiwa hoja hizo za makubaliano ya MAL na Apex yalikuwa yametiwa sahihi na Lawrence Litein Shoona.
Mshtakiwa alidaiwa alimkabidhi msajili wa makampuni (BRS) hoja hizo feki za kutwaa mali ya Shoona iliyoko kwenye MAL hadi Apex.
Shtaka la tano lilisema Njoroge akiwa mkurugenzi wa MAL aliiba mali zote za marehemu zenye thamani ya Sh25milioni.
Njoroge aliomba aachiliwe kwa dhamana akiapa kufika kortini wakati wa kusikizwa kwa kesi inayomkabili.
Upande wa mashtaka ulisema haupingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.
Hakimu alimwagiza Njoroge awasilishe kortini dhamana ya pesa tasilimu Sh500,000.
Upande wa mashtaka uliamriwa umkabidhi mshtakiwa nakala za mashahidi aanze kuandaa tetezi za ushahidi wake.
Mshtakiwa alielezwa atarudi tena kortini mnamo Novemba 13,2025 kufahamishwa siku ya kusikizwa kwa kesi hiyo inayomkabili.
Pia hakimu aliamuru kiongozi wa mashtaka pamoja na polisi wamkabidhi mshtakiwa taarifa za mashahidi ndipo abaini mashahidi atakao waita kumtetea katika jitihada zake za kujinasua.
Mshtakiwa hakuweza kulipa dhamana hiyo mara moja.
Alipelekwa kizuizini hadi wakati ule atakapolipa dhamana hiyo.