Dimba

Halaand ampiku Ronaldo kwa kufungia timu tatu tofauti mabao matano mfululizo

Na MASHIRIKA November 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MVAMIZI matata Erling Haaland ameweka historia mpya kwenye Klabu Bingwa Ulaya kwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao katika mechi tano mfululizo akiwa na timu tatu tofauti.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amekuwa katika kiwango cha juu msimu 2025–2026 akichezea Manchester City na timu ya taifa ya Norway.

Mnamo Novemba 5, 2025, alifunga bao dhidi ya timu yake ya zamani Borussia Dortmund uwanjani Etihad baada ya dakika 29 tu. Bao hilo lilikuwa la “mtindo wa Haaland”, akimalizia kwa nguvu krosi ya chini kutoka upande wa kushoto, dakika saba baada ya Phil Foden kufungua ukurasa wa mabao.

Foden aliongeza bao la tatu dakika ya 57, kabla ya Rayan Cherki kufunga la nne katika dakika za majeruhi, huku Waldemar Anton akipachika bao la Dortmund kufutia machozi.

Bao hilo lilikuwa la 18 kwa Haaland msimu huu katika mashindano yote, akiwa amesakata mechi 14 tu, na kukosa kufunga katika michezo miwili pekee (dhidi ya Tottenham Hotspur na Aston Villa).

Katika timu ya taifa ya Norway, Halaand amefunga mabao tisa katika mechi tatu za mwisho, akiiongoza kuimarisha nafasi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1998.

Bao lake dhidi ya Dortmund limemweka kwenye vitabu vya historia ya Klabu Bingwa Ulaya — rekodi ambayo hata mshambulizi matata wa Ureno, Cristiano Ronaldo hakuwahi kuifikia akiwa Manchester United, Real Madrid au Juventus. Hiyo ilikuwa mechi ya tano mfululizo ambayo Haaland amefunga kwenye mashindano hayo tangu msimu uliopita.

Safari yake ya kwanza ya kufunga mabao katika michuano michuano mitano mfululizo ilianza akiwa na Salzburg nchini Austria kati ya Septemba na Novemba 2019, alipofunga mabao manane kabla ya kuhamia Dortmund mnamo Januari 2020. Msimu wa 2020-2021 akiwa na Dortmund, alifunga mabao 10 katika mechi sita mfululizo.

Iwapo atafunga tena katika mchezo ujao wa City dhidi ya Bayer Leverkusen, atafikia rekodi yake binafsi aliyoiweka akiwa na Dortmund. Hadi sasa, Haaland amefunga mabao mawili katika mipepetano mitatu dhidi ya Dortmund, likiwemo goli alilopachika Septemba 2022.

Ushindi dhidi ya Dortmund unaweza kuiweka City kileleni mwa ligi hiyo ya timu 36, huku wakiwa miongoni mwa klabu ambazo hazijapoteza mechi msimu huu kwenye Klabu Bingwa Ulaya kama Arsenal, Bayern Munich, Inter Milan na Tottenham.

Haaland sasa anatarajia kuendeleza makali yake katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Liverpool hapo Novemba 9, ingawa amewahi kuwafunga mara moja pekee katika mechi nne zilizopita za ligi dhidi yao.

Imetafsiriwa na Geoffrey Anene