Uhuru amtetea Gachagua, akemea Kioni
RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta amemtetea aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, akionya viongozi wa chama chake cha Jubilee dhidi ya kumtukana kiongozi huyo.
Akizungumza Ijumaa, Novemba 7, 2025 alasiri katika Kaunti ya Murang’a wakati wa mkutano wa mashinani wa chama hicho, Bw Kenyatta alisema amesikitishwa na kile alichokitaja kama siasa za mgawanyiko na matusi zinazopendwa na baadhi ya maafisa wa chama chake.
Rais huyo mstaafu aliwataka wanachama wa Jubilee kuacha mara moja tabia ya kutumia mitandao ya kijamii kwa lugha za kudhalilisha na badala yake waendeleze mijadala ya heshima na kujenga chama kupitia hoja.
“Wakati mwingine huwa ninahuzunika kuona watu mitandaoni wakidai kutetea chama kwa kumtukana Rigathi Gachagua na wengine. Sitaki upuuzi kama huo ndani ya chama changu. Watu wafanye siasa kwa heshima,” alisema Bw Kenyatta.
Aliendelea:“Ni aibu kwamba wengi wao ni maafisa wa chama. Nasisitiza kabla sijakabidhi chama hiki rasmi, nikiona wanaendelea na tabia hiyo, sitasita kuwakemea hadharani na kuwafurusha. Sitaki kusikia mambo hayo tena.”
Bw Kenyatta alimkemea hadharani Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, akimtaka aache mara moja kuwaongoza wanachama wengine kumshambulia Bw Gachagua.
Aliwataka viongozi wote wa chama hicho kuelekeza nguvu zao katika kusambaza sera na malengo ya Jubilee, badala ya kutumia muda mwingi kutukana viongozi wengine mitandaoni.
“Wacheni mambo ya lawama na majibizano. Kiongozi wa kweli ni yule anayeeneza sera, si matusi. Tukubaliane kwamba Jubilee si chama cha matusi,” alisisitiza.
Katika mkutano huo wa mashinani, Bw Kenyatta pia aliendelea kumpigia debe aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, akimtaja kama kiongozi mwenye maono na mchapakazi anayestahili kupewa nafasi ya juu zaidi ya uongozi wa taifa.
“Nimefanya kazi na Dkt Matiang’i. Ni mtu anayependa kazi na anayeleta matokeo. Si suala la upendeleo binafsi, bali ni kwa sababu natambua uwezo wake wa kuleta mabadiliko,” alisema Bw Kenyatta.
Hata hivyo, alikanusha madai kwamba kumuunga mkono Dkt Matiang’i kumetokana na urafiki wao wa karibu, akisema kwamba anamuunga mkono kutokana na rekodi yake wakati wa serikali iliyopita.
Kauli ya Bw Kenyatta inajiri mwezi mmoja baada ya Jeremiah Kioni kumshambulia Bw Gachagua, akimlaumu kwa kudhulumu mgombea urais wa chama hicho, Dkt Matiang’i.