Makala

Umuhimu wa upasuaji wa maiti kwa haki na uwajibikaji

Na Steve Otieno November 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MTU anapokufa akiwa chini ya ulinzi wa polisi au wakati wa maandamano, kugundua jinsi alivyokufa kunaweza kuamua iwapo haki itatendeka au wahusika wataepuka adhabu.

Uchunguzi wa kitaalamu, hasa uchunguzi wa kina wa maiti, ndio ufunguo wa ukweli huo.

Hii ni kulingana na wataalamu wa kimataifa waliotembelea Kenya wiki hii na kuhimiza serikali kuimarisha viwango vya uchunguzi wa kisayansi vinavyotumika katika uchunguzi wa vifo vya wafungwa, wanaoteswa, na waathiriwa wa mauaji ya kiholela.

Walisema uchunguzi unaotegemea sayansi pekee ndio unaweza kuhakikisha uwajibikaji na kurejesha imani ya umma katika mfumo wa haki.

Profesa Djordje Alempijevic, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Tiba katika Chuo Kikuu cha Belgrade na mwanachama wa Kamati Ndogo ya Umoja wa Mataifa kuhusu Kuzuia Mateso, alisema ushahidi wa kitaalamu bado ndio njia ya kuaminika zaidi kuelekea ukweli na haki.

“Ukweli ni muhimu kwa maridhiano, kufungwa kwa kesi, na haki. Uchunguzi huu unatoa ukweli unaothibitishwa na usioegemea upande wowote,” alisema.

Profesa Alempijevic alibainisha kuwa ingawa madaktari  na  wanapatholojia wa Kenya wanajitahidi, ripoti nyingi za uchunguzi wa maiti bado hazikidhi viwango vya kimataifa kama ilivyoainishwa katika Itifaki ya Minnesota kuhusu Uchunguzi wa vifo vinavyoweza kutokea kinyume cha sheria.

Alionya kuwa ukosefu wa uthibitisho sahihi unaharibu uchunguzi na kuchelewesha haki.

“Kile ambacho wanapatholojia wa Kenya wanaona kwenye meza ya uchunguzi lazima kiandikwe kwa usahihi kiasi kwamba mtaalamu yeyote wa kiwango hicho anaweza kurudia matokeo,” alisema.

Kwa Profesa James Lin, Mratibu wa  Mipango ya Itifaki ya Istanbul katika Baraza la Kimataifa la Urejeshaji kwa Waathiriwa wa Mateso (IRCT), alisema uchunguzi wa aina hii unaondoa dosari na upendeleo katika uchunguzi.

“Njia pekee ya kuhakikisha uwajibikaji na uwazi ni kutumia mbinu zinazotegemea sayansi. Familia zinastahili kujua kilichotokea kwa wapendwa wao, na jamii inastahili kuona haki ikitendeka. Uchunguzi lazima utegemee ushahidi, si maoni au siasa,” alisema Prof Lin.

Aliongeza kuwa kuimarisha uwezo wa uchunguzi wa maiti Kenya kutahakikisha kila hatua, kuanzia kurekodi sehemu za uhalifu hadi kufanya uchunguzi wa maiti, inatimiza mbinu bora za kimataifa. Ubora huu, alisema, utaimarisha imani ya umma na kufanya iwe ngumu kwa watenda uhalifu kuepuka uwajibikaji.