Wanaharakati Njagi na Oyoo wasimulia walivyoteswa na jeshi la Uganda kwa siku 38
Wanaharakati wa Kenya, Bob Njagi na Nick Oyoo, wamesema waliteswa na kutendewa unyama kwa siku 38 wakiwa kizuizini katika kambi ya jeshi nchini Uganda licha ya serikali ya nchi hiyo kukanusha ilikuwa imewazuilia.
Mnamo Oktoba 14, Mahakama Kuu ya Kampala iliamuru serikali ya Uganda iwasilishe wawili hao wakiwa “hai au wafu” ndani ya siku saba. Hata hivyo, majibu ya serikali yalieleza kuwa Jeshi la Ulinzi la Watu wa Uganda (UPDF) lilikagua vituo vyote lakini halikuweza kupata rekodi yoyote ya Njagi au Oyoo.
Jana walipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, walionekana wazi wazi kuwa wameathirika. Miili yao ilikuwa dhaifu, mabega yalikuwa yameshuka, na mwendo wao ulikuwa polepole, kana kwamba kila hatua ilikuwa inahitaji juhudi maalum. Sauti zao zilikuwa za chini zikiwa na uzito wa maumivu ya kiakili kutokana na kile walichosema walikumbana nacho wakizuiliwa na jeshi lUganda.
‘Siku 38 za kutekwa si rahisi, tulitekwa na jeshi na tukawekwa chini ya amri maalum ya jeshi la Uganda. Imekuwa ngumu. Tuliteswa na kutendewa unyama. Mimi mwenyewe si kula kwa siku 14, nilikuwa nafunga,’ alisema Bob Njagi. Oyoo alisema ‘wameathirika kiakili, lakini wanafurahi kurudi nyumbani’ baada ya kipindi kigumu wakiwa ugenini.
“Kwa sasa hatutaki kusema mengi kwa sababu tunahitaji matibabu. Tumeathirika kiakili, lakini tunafurahi kurudi nyumbani. Ni furaha kuwa hapa,” alisema Oyoo.
‘Kuna mambo ambayo pengine niliyachukulia kawaida. Leo, huenda sitayachukulia kama kawaida. Na naamini huu ni wakati na yote hayo ni hatua zinazonipeleka mbele,’ aliongeza
Nje ya uwanja wa ndege, wanaharakati walikusanyika na kuanza kuimba wimbo wa taifa, kisha walijikuta wakisema ‘Aibu kwako Museveni,’ wakimlenga Rais wa Uganda.
Amnesty International ilieleza kuwa kuachiliwa kwa wanaharakati hao kulifuatia majadiliano ya ngazi za juu, ikiwa ni pamoja na kuingilia kati kwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Mkurugenzi Mtendaji wa Amnesty International Kenya, Irungu Houghton alionya kuhusu mwelekeo unaotia wasiwasi Tanzania na Uganda unaonyesha hatari inayoendelea dhidi ya haki za binadamu, ambao unaweza kuathiri uchaguzi wa 2026 nchini Uganda na uchaguzi wa 2027 nchini Kenya.
“Tunaomba watu wote katika Afrika Mashariki kutoa sauti zao. Watazania wameonyesha ujasiri licha ya vitisho, na Waganda na Wakenya lazima wafanye vivyo hivyo. Kwa mshikamano, watu wa Afrika Mashariki lazima wahakikishe kwamba uchaguzi ni wa huru, wa haki, na wa kidemokrasia,” alisema.
Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni, Dkt Korir Sing’oei alithibitisha Jumamosi kwamba Bob Njagi na Nicholas Oyoo waliachiliwa Ijumaa usiku na tayari walikuwa wamefika Kenya.
“Bob Njagi na Nicholas Oyoo wako huru na wako katika ardhi ya Kenya,” alisema Dkt Sing’oei. “Usiku wa jana, baada ya majadiliano marefu, wawili hao walikabidhiwa balozi wetu Uganda, Joash Maangi. Waliambatana na Balozi na maafisa wa serikali ya Uganda hadi mpaka wa Busia, ambapo walipokelewa na Kamishna wa Kaunti ya Busia, Chaunga Mwachaunga.”
Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Kenya, alikuwa ameandikia rasmi Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Uganda, Jenerali Jeje Odongo akitaka maelezo na kuhimiza nchi hiyo kuchukua hatua haraka kutafuta wawili hao.
Katika barua iliyoandikwa Oktoba 31, 2025, Mudavadi alionyesha hasira yake kutokana na kimya cha Uganda licha ya mawasiliano ya kidiplomasia na simu kati ya maafisa wa nchi zote mbili.