Makala

Sababu za Trump kumtuma makamu wake kwa Ruto

Na JUSTUS OCHIENG, BENSON MATHEKA November 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Ziara hiyo, inayotarajiwa kufanyika kati ya Novemba 25 na 30, inajiri katika kipindi nyeti kwa uhusiano wa kibiashara na kiusalama kati ya Kenya na Amerika, huku serikali ya Rais Ruto ikitumaini kufufua uhusiano wa karibu ulioshuhudiwa mwishoni mwa utawala wa aliyekuwa Rais Joe Biden.

Ingawa Ikulu ya Nairobi imekuwa kimya kuhusu maelezo ya ziara hiyo, mazungumzo ya ngazi ya juu yamekuwa yakiendelea kati ya maafisa wakuu wa serikali za nchi hizo mbili. Wajumbe wa kidiplomasia wamekuwa wakipitia makubaliano ya kina ya ushirikiano yaliyotiwa saini Mei 2024, wakati wa ziara ya Rais Ruto nchini Amerika.

Makubaliano hayo yanahusu biashara, uwekezaji, teknolojia, utawala bora, mabadiliko ya tabianchi na usalama wa kikanda.“Kwa mwaka uliopita, ahadi nyingi zilizotolewa sasa zimeanza kutekelezwa kwa vitendo na maendeleo ni ya kuridhisha,” alisema Waziri wa Masuala ya Kigeni na Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi.

“Kenya inasalia kuwa mshirika muhimu wa Amerika barani Afrika, bila kuathiriwa na mabadiliko ya kisiasa yaliofanyika Washington.”Katibu katika Wizara ya Masuala ya Kigeni, Dkt Korir Sing’oei, alisema ziara ya Bw Vance inaonyesha uthabiti wa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili na mwendelezo wa mazungumzo yaliyoanza baada ya ziara ya kihistoria ya Rais Ruto Mei mwaka jana,heshima ambayo haikuwa imetolewa kwa kiongozi yeyote wa Afrika kwa zaidi ya miaka 20.

Katika ziara hiyo, Kenya ilipandishwa hadhi na kutambuliwa rasmi kama “Mshirika Mkuu wa Amerika asiye mwanachama wa NATO” (MNNA), taifa la kwanza kusini mwa Jangwa la Sahara kupata hadhi hiyo. Uteuzi huo unaiweka Kenya katika nafasi ya kipekee kama mshirika wa karibu wa Amerika katika masuala ya kijeshi na kiusalama duniani.Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa chama cha Republican wamependekeza hadhi hiyo ipitiwe upya, wakitaja uhusiano wa Kenya na China, Urusi, na Iran.

Mwezi Agosti, Seneta Jim Risch aliwasilisha mswada bungeni kutaka kufanyiwa tathmini upya nafasi ya Kenya kama MNNA, akitaja biashara yake na mataifa hayo na tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu.

Waziri Mudavadi alidhibitisha taharuki hiyo, akisisitiza kuwa ushirikiano wa Nairobi na Washington umeendelea vizuri licha ya mabadiliko ya kiutawala, huku akiongeza kwamba mazungumzo mapya sasa yanajumuisha “teknolojia ya utengenezaji wa vipuri vya kielektroniki na madini adimu duniani.”

Biashara pia itakuwa ajenda kuu ya mazungumzo hayo. Kwa kuwa Mkataba wa AGOA (African Growth and Opportunity Act) unatarajiwa kuisha muda wake mwezi Septemba 2026, Kenya imeanza mazungumzo ya pande mbili na Amerika kuhusu mfumo mpya wa biashara.AGOA, uliodumu kwa miaka 25, umekuwa ukiruhusu bidhaa za Kenya kuuzwa Amerika bila ushuru.

Utawala wa Rais Donald Trump uliongeza mpango huo kwa mwaka mmoja ili Kenya iweze kujadiliana upya kuhusu makubaliano mapya ya muda mrefu.

“Iwapo Amerika haitadumisha AGOA kwa nchi zote, basi kila nchi italazimika kujadiliana masharti yake binafsi,” alisema Mudavadi.Ajenda nyingine muhimu wakati wa ziara ya Bw Vance ni kuhusu Operesheni ya Amani nchini Haiti, ambapo Kenya imetuma maafisa wa polisi 800 kusaidia kurejesha utulivu. Hata hivyo, mpango

huo unakabiliwa na ukosefu wa ufadhili baada ya Amerika kuashiria huenda ikasitisha mchango wake wa dola milioni 200 hadi Umoja wa Mataifa utoe idhini zaidi.

Ziara ya Bw Vance pia inafanyika wakati ambapo Washington ina wasiwasi kuhusu ushawishi unaoongezeka wa China barani Afrika, hasa baada ya ziara ya Rais Ruto nchini Beijing mwezi Aprili, ambapo yeye na Rais Xi Jinping walikubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kiteknolojia.Kwa mujibu wa wachambuzi, ziara hiyo ya Vance italenga “kuhakikisha Kenya inasalia kuwa nguzo ya kimkakati ya Amerika” katika bara la Afrika, hususan katika nyanja za biashara, ulinzi na usalama wa kikanda.