Makala

Gachagua akiri kwamba alikuwa akimkaidi Ruto peupe

Na  MWANGI MUIRURI November 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amezua mjadala mkali baada ya kufichua aliyopitia akiwa msaidizi wa Rais William Ruto, akieleza wazi kuwa mara kadhaa alipuuza maagizo ya rais na kukataa kuyatekeleza.

Akizungumza Ijumaa jijini Nairobi wakati wa uzinduzi wa kitabu The Fight for Order kilichoandikwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Gachagua alisema aliamini jukumu lake halikuwa tu kusaidia rais, bali pia “kumrekebisha” pale ambapo alihisi mambo hayaendi sawa.

“Nilikuwa mtu pekee mwenye ujasiri wa kumkosoa Rais Ruto. Nilikataa maagizo yake kadhaa pale nilipoona hayakuwa sahihi,” alisema Gachagua huku akiwashangaza waliohudhuria hafla hiyo.

Kulingana na Gachagua, kulikuwa na nyakati alihisi kuwa yeye ni “rais mwenza” mwenye mamlaka ya kusimamia baadhi ya maamuzi ya serikali. Alisema mara nyingi alikataa maagizo aliyohisi “hayakulingana na maoni” yake.

Baada ya kuondolewa madarakani kupitia mchakato wa Bunge Oktoba 2024, Rais Ruto alimteua Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais mpya. Wakati wa kumuapisha mnamo Novemba 1, 2025, Rais Ruto alisema Nataka uwe Naibu Rais ambaye sikuwahi kuwa naye kwa miaka miwili iliyopita,mtiifu, mchapakazi, na mwenye kuelewa majukumu yake.”

Gachagua pia alisimulia tukio lililotokea baada ya maandamano ya vijana wa Gen Z mnamo Juni 2024, ambapo Rais Ruto alivunja Baraza la Mawaziri. Alisema kuwa wakati wa kuunda upya serikali, rais alijaribu kushirikisha viongozi wa upinzani akiwemo Raila Odinga.

“Nilimruhusu aendelee na maamuzi yake, lakini nilishtuka alipotangaza majina ya mawaziri wapya bila kujumuisha yeyote kutoka Embu. Nilimuuliza kwa nini, akaniambia nisubiri,” alisema.

Aliongeza kuwa Rais alimwita yeye na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi wamsindikize wakati wa kutangaza baraza jipya, lakini alikataa.

“Nilimuuliza: ‘Tutakusindikiza kutangaza majina tusiyoyajua?’ Nikakataa kabisa,” alisema Gachagua.

Alidai kuwa Rais alikasirika sana, akaingia ofisini kwake na kurudi akiwa amebadilisha jina la aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, akimteua mtu mwingine aliyechaguliwa kwa ushawishi wa Gavana Cecily Mbarire wa Embu.

“Nilimwambia siwezi kukubali. Nilimkumbusha kuwa tayari alikuwa amemteua mtu kutoka Meru bila kuniuliza, na sasa anafanya vivyo hivyo tena,” alisema Gachagua.

Kwa mujibu wake, Rais Ruto alinyamaza kwa muda wa dakika tatu kabla ya kumwambia abadilishe jina hilo na kumrudisha Muturi.

“Nilimwambia nikienda jukwaani na kuthubutu kutangaza jina jipya, ningeondoka hadharani mbele ya kamera,” alisema. “Hivyo ndivyo nilivyookoa kazi ya Muturi, lakini baada ya miezi mitatu, nikatupwa nje serikalini. Muturi naye akafutwa kazi muda mfupi baadaye.”

Wakati Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse alipowasilisha hoja ya kumuondoa Gachagua bungeni, miongoni mwa mashitaka yaliyomkabili yalihusu “kumdhalilisha rais, kupuuza baraza la mawaziri, na kuendeleza ukabila na upendeleo wa kisiasa.”

Katika simulizi nyingine, Gachagua alisema alihusishwa moja kwa moja na tukio la kutekwa kwa mtoto wa Muturi, akidai alisaidia kumrejesha nyumbani baada ya kumtaka Muturi amkabili Rais ana kwa ana.

“Nilimpigia Rais na nikajua anajua mtoto huyo alikokuwa. Nilimwambia Muturi amkabili ikulu, na ndani ya saa mbili mtoto wake alirudi,” alisema.

Gachagua alikiri pia kwamba wakati wa mikutano ya ndani ya serikali, alikuwa na mbinu ya kuepuka kufikiwa na Rais.

“Rais alikuwa na tabia ya kuwatuma mawaziri kuniletea maagizo, lakini nilikuwa naacha simu ofisini ili nisiweze kupatikana,” alisema huku umati ukicheka.

Gachagua alisema alipinga vikali Mswada wa Fedha wa 2024, uliosababisha maandamano ya Gen Z, akisisitiza kuwa alikuwa upande wa vijana.

“Nilimuambia Rais kuwa wale hawakuwa magaidi kama alivyosema. Ni watoto wetu wanaotaka kusikizwa,” alisema.

Baada ya Rais kuhutubia taifa akiwalaumu waandamanaji, Gachagua naye alitoa hotuba dakika chache baadaye, akisema hawakuwa wahalifu mbali vijana waliokuwa wakipigania haki yao.

Kwa sasa, Gachagua ni kiongozi wa chama kipya Democracy for Citizens Party (DCP) na amesema atakitumia kupigania demokrasia ya kweli na uwajibikaji serikalini.”

Kauli zake zimeibua hisia kali, huku wandani wa Rais Ruto wakisema amedhihirisha ni “tishio kwa usalama wa taifa.”

“Umesikia mwenyewe akisema alikuwa anampinga rais na hata kumfanya aonekane mdogo mbele yake. Hiyo ndiyo sababu alipaswa kuondolewa madarakani,” alisema Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri.