Jamvi La Siasa

Wamuchomba afokea Gachagua kuhusu ‘tugege’ na chama cha ‘masikio

Na  BENSON MATHEKA November 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Githunguri, Gathoni Wamuchomba, ameimarisha ukosoaji wake dhidi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na chama chake cha Democracy for Citizens (DCP), akiapa wazi kwamba hatajiunga na chama hicho.

Bi Wamuchomba aliamua kutumia mitandao yake ya kijamii kushambulia Gachagua na chama chake cha DCP akikitaja kama “chama cha masikio” kutokana na alama yake ya mkono unaokinga sikio kuashiria kauli mbiu yake ya ‘Skiza ground’.

Alidai kuwa wanachama wa chama hicho mara kwa mara hulaumu viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya waliokataa kujiunga nacho wakiwaita “wajinga” na “waovu.”

Mbunge huyo alikumbuka hali ambapo kabla ya uchaguzi wa 2022 viongozi wa eneo la Mlima Kenya walikaidi Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alipowaonya wakazi dhidi ya kumchagua William Ruto na naibu wake, Rigathi Gachagua.

Kulingana na Wamuchomba, wengi walipuuza onyo la Uhuru, wakimtaka amalize muhula wake na kuondoka madarakani.Hata hivyo, alidai kuwa onyo hilo limekuja kutimia, akitaja mzigo wa ushuru, kuporomoka kwa biashara, kubomolewa kwa nyumba, kupungua kwa bonasi ya chai na vifo vya vijana kama matokeo ya maamuzi yaliyofanywa na viongozi kukaidi Rais Uhuru 2022.

Akijibu kauli za hivi karibuni za Gachagua kuhusu mbunge wa Kiambaa, John Kawanjiku, ambaye aliunga mkono kampeni zake akachaguliwa 2021, akimtaja kama “kagege”, Wamuchomba alisema badala ya naibu rais wa zamani kushughulikia maslahi ya watu wa Mlima Kenya, kama vile mabadiliko ya sekta ya chai, anashughulika kutukana watoto wa wake wasio katika ndoa.

“Kikosi cha hasira kimerudi tena, kikitukana kila anayekataa kujiunga na chama cha ‘Maskio’. Siasa za hisia ni hatari. Alisema kuwa anaitwa fuko kwa sababu ya kuambia ukweli walio mamlakani lakini akasisitiza kwamba ataendelea kusema ukweli usiopendeza watawala.

Mbunge huyo alitangaza kwamba hataunga mkono viongozi wasio wasafi na akaahidi kwamba hatajiunga na DCP bila kujua chama hicho kinasimamia nini au kwa sababu ya hofu.

“Sitaunga mkono muuaji, na nimekuwa thabiti, lakini sitajiunga na chama cha ‘Masikio’ kwa sababu ya vitisho,” aliongeza.