Jamvi La Siasa

Sababu za Kalonzo na Gachagua kumezea mate Orengo

Na JUSTUS OCHIENG, BENSON MATHEKA November 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Muungano wa Upinzani unaoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka unawania kumteua Gavana wa Siaya, James Orengo, kuwa mmoja wa vinara ili kuvutia uungwaji mkono kutoka  eneo la Luo Nyanza.

Vyanzo vya ndani ya muungano huo viliambia Taifa Jumapili kwamba Gavana Orengo anamezewa mate na  upinzani kutokana na uzoefu wake wa kisiasa na msimamo thabiti kuhusu uhusiano wa chama cha ODM na serikali jumuishi.

Vyanzo  vimefichua kuwa  Bw Orengo anawaziwa  kuwa mgombea mwenza katika muungano mpya wa Upinzani unaoleta pamoja aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Martha Karua wa Chama cha People’s Liberation Party, Eugene Wamalwa wa DAP-Kenya, Justin Muturi wa Chama cha Democratic Party, na chama cha Jubilee cha Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kinachowakilishwa na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i.

Hata hivyo, kwa Orengo, kujiunga na muungano kama huo kutakuwa ni Kamari hatari ya kisiasa ikiwa eneo la Nyanza litaamua kubaki na Rais William Ruto katika mfumo wa serikali jumuishi. Kaimu  Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga, amesisitiza kwamba mustakabali wa kisiasa wa eneo hilo bado uko wazi, na kwamba chama hakiwezi kukubali chochote chini unaibu rais katika uchaguzi wa 2027 iwapo kitaungana na vingine.

Orengo ni miongoni mwa washirika wa karibu wa aliyekuwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ambao wameonyesha kuwa wangeachana na Rais Ruto na badala yake kushirikiana na Bw Musyoka katika uchaguzi wa rais wa 2027.

Katika ishara ya shukrani kwa mtu ambaye alisimama na Odinga kwa sehemu kubwa ya safari yake ya kisiasa, baadhi ya wanajamii wa familia ya Odinga, wakiongozwa na dada wa Odinga na Mbunge wa Kisumu, Ruth Odinga, mjane Ida Odinga, na Bw Orengo, wanamuona Bw Musyoka kama mtu anayeweza kuaminika kuendeleza urithi wa kiongozi huyo wa ODM.

Hii inaweza kuwa pigo kwa Rais Ruto, ambaye anatarajia kurithi wafuasi wa Odinga kufuatia makubaliano kati ya viongozi hawa wawili yaliyosababisha kuundwa kwa serikali pana.

Katika ziara ya ujumbe wa Wiper katika shamba la Opoda na Kang’o ka Jaramogi huko Bondo Alhamisi, viongozi walimiminia sifa Bw Musyoka. Ziara hiyo ilikuwa ya kibinafsi na ya ishara: ziara ya kumheshimu mtu ambaye Bw Musyoka alimtaja kama “ndugu, mwenza kwenye mapambano, na kamanda ambaye aliyepaswa kuwa kiongozi waJamhuri ya Kenya.”