Imani za kidini si mipaka ya ndoa nchini Kenya
Katika ulimwengu wa sasa ndoa kati ya watu wa imani tofauti zimeongezeka.
Jamii inaendelea kuwa wazi na kuvumilia tofauti za kidini na kitamaduni na Kenya pia imeshuhudia ongezeko la ndoa za aina hii.
Ndoa hizi haziunganishi tu watu binafsi, bali pia zinaakisi roho ya uvumilivu, uhuru wa kidini na utofauti ulioainishwa katika Katiba ya Kenya ya mwaka 2010.
Kifungu cha 3 cha Sheria ya Ndoa 2014 kinafafanua ndoa kuwa ni “muungano wa hiari kati ya mwanaume na mwanamke, iwe ya mke mmoja au wake wengi, na uliosajiliwa kulingana na sheria.” Hapam haiweki mipaka ya kidini.
Wanandoa wote wana haki sawa wakati wa ndoa, katika maisha ya ndoa na hata wakati wa kuvunjika kwake.
Umri wa chini wa kuingia kwenye ndoa ni miaka 18, na ndoa yoyote chini ya umri huo ni kosa la jinai. Hapa pia, haiweki mipaka yoyote ya kidini.
Kifungu cha 6 cha Sheria ya Ndoa kinatambua ndoa tano kuu:Ndoa ya Kikristo,Ndoa ya Kiraia,Ndoa ya Kitamaduni, Ndoa ya Kihindu, Ndoa ya Kiislamu.
Ndoa za Kikristo, Kihindu na Kiraia ni za mke mmoja, ilhali ndoa za Kitamaduni na Kiislamu zinaweza kuruhusu wake wengi.
Hata hivyo, mahakama zimeeleza kwamba orodha hii si ya mwisho; kuweka dini zinazotambuliwa kisheria kuhusu ndoa ni kinyume cha Katiba, hasa Ibara ya 27 (usawa na uhuru dhidi ya ubaguzi) na Ibara ya 32 (uhuru wa dini na imani).
Wanandoa lazima wawe na umri wa miaka 18 au zaidi, wawe wameridhia ndoa kwa hiari, wawe na mashahidi wawili wenye akili timamu, na kila mmoja awe hana ndoa nyingine halali.
Stakabadhi kama vitambulisho, vyeti vya kuzaliwa, na kiapo cha kutokuwa kwenye ndoa nyingine ni muhimu.
Katika kesi ya Mary Wanjuhi Muigai dhidi ya Mwanasheria Mkuu & mwingine ya 2015 ilivyoripotiwa katika Kenya Law Reporting( eKLR), mahakama iliamua kwamba Kifungu cha 6 cha Sheria ya Ndoa kina mapungufu kwa kutotambua ndoa za dini zingine.
Mahakama iliagiza kifungu hicho kiwe kwa namna inayojumuisha dini zote zilizosajiliwa nchini.
Kifungu cha 52 na 93 cha Sheria ya Ndoa kinawaruhusu viongozi wa dini zisizo za Kikristo, Kiislamu au Kihindu kuomba usajili kwa Msajili wa Ndoa ili waruhusiwe kuongoza ndoa kwa mujibu wa imani zao.
Hii inahakikisha waumini wa dini zote wanaweza kufunga ndoa kihalali bila kubaguliwa.
Wapenzi wa dini tofauti wanaweza kuchagua kufunga ndoa kwa njia mbili:Ndoa ya Kiraia, inayoendeshwa na Msajili katika ofisi za Mwanasheria Mkuu, yenye mwelekeo wa kidunia na inatambulika kisheria na Ndoa ya Kidini, ambapo kiongozi wa dini aliyesajiliwa anaweza kufungisha ndoa hiyo chini ya sheria.
Katiba ya Kenya, 2010, inasisitiza ujumuishaji na heshima kwa dini zote katika kufunga ndoa. Kwa mujibu wa vifungu vya 52 na 93, viongozi wa dini yoyote wanaweza kusajiliwa ili kufungisha ndoa, kuhakikisha usawa wa kidini na kutekeleza matakwa ya Ibara ya 27 na 32 za Katiba.