Jamvi La Siasa

Ni wazi Khalwale na Ruto wameshibana

Na CHARLES WASONGA November 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SENETA wa Kakamega, Boni Khalwale, kwa mara nyingine ameonyesha ishara ya kumtoroka Rais William Ruto kuelekea uchaguzi mkuu ujao alipodinda kuandamana naye wakati wa ziara yake katika kaunti hiyo na eneo la magharibi kwa ujumla.

Kabla ya ziara ya Dkt Ruto ya siku nne iliyokamilika Jumamosi, Novemba 1, 2025, Dkt Khalwale, ambaye ni kiranja wa wengi katika Seneti, alijitokeza waziwazi kumuunga mkono mgombea wa muungano wa upinzani Seth Panyako katika uchaguzi mdogo wa Malava utakaofanyika tarehe 27 mwezi huu.

Mnamo Novemba 7, 2025, seneta huyo wa Kakamega pia alikosa kuhudhuria shughuli ya uzinduzi wa usambazaji wa fedha za mpango wa kitaifa wa kuwawezesha vijana (NYOTA) katika uwanja wa michezo wa Mumias, kaunti ya Kakamega.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa hatua hiyo itakuwa pigo kubwa kwa Dkt Ruto katika jitihada zake za kurithi kaunti ya Kakamega, kisiasa, baada ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Katika chaguzi zilizopita za urais, ukiwemo uchaguzi wa mwaka jana, marehemu Raila amekuwa akipata kura nyingine zaidi katika kaunti ya Kakamega kuliko wagombeaji wengine wa urais.

Kwa mfano, katika uchaguzu mkuu wa 2022, Raila alipata jumla ya kura 357,826 katika kaunti hiyo huku Rais Ruto akipata kura 140, 626, kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Isitoshe, kati ya maeneo bunge 12 karika kaunti ya Kakamega, maeneo bunge tisa yanawakilishwa na wabunge waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM.

Katika ngazi ya kaunti, isipokuwa Seneta Khalwale aliyeibuka mshindi kwa tiketi ya chama cha UDA, ODM ilitwa viti vya ugavana na mbunge mwakilishi wa kaunti ambao ni; Ferdindand Barasa na Bi Elsie Muhanda, mtawalia.

Hii ndio maana hatua ya Dkt Khalwale kugeuka mkosoaji wa serikali ya Rais Ruto na kumuunga mkono Bw Panyako imemweka katika hatari ya kuadhibiwa na chama chake cha United Development Alliance (UDA) kwa kukiuka Katiba yake na Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2024.

Kati ya adhabu hizo ni kutimuliwa kutoka chama hicho tawala na hivyo kupoteza kiti chake cha useneta wa Kakamega.

Katika barua aliyoandikiwa Oktoba 9, 2025 na kutimwa saini na mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya UDA Charles Njenga, chama hicho kilisema kimepokea ushahidi kwamba Khalwale alishiriki katika kampeni za Bw Panyako anayegombea kiti cha ubunge cha Malava kwa tiketi ya DAP-K badala ya mgombeaji wa UDA David Ndakwa.

“Hii ni kinyume cha Katiba ya UDA iliyokudhamini katika Seneti sawa na Sehemu ya 14 ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2024,” ikasema barua hiyo.

Seneta Khalwale alipewa muda wa siku 14 kujitetea kuhusu tuhuma hizo la sivyo, achukuliwe hatua za kinidhamu, ikiwemo kusimamishwa kwa muda au kutimuliwa kutoka UDA.

Lakini kwenye mahojiano na safu hii, Seneta Khalwale alisema anamuunga mkono Bw Panyako kwa sababu ndiye mgombeaji bora zaidi na “atakayeendeleza umoja wa jamii ya Waluhya”.

“Namuunga mkono Bw Panyako kwa sababu ndiye mwenye uungwaji mkubwa na anayebeba matamanio ya watu wa Malava. Chama cha UDA kilifaa kumuunga mkono mgombea huyo kwa sababu katika uchaguzi mkuu wa 2022, ndiye alikuwa wa pili kwa karibu zaidi nyumba ya marehemu Malulu Injendi,” anaeleza.

Hata hivyo, tangu Januari mwaka huu, Seneta Khalwale amegeuka kuwa mpinzani wa serikali anayoitumikia katika Seneta kama kiranja wa wengi.

Mnamo Aprili 7, mwanasiasa huyo alihutubia kikao cha wanahabari nyumbani kwake Malinya, eneo bunge la Ikolomani, ambapo aliilaumu serikali ya Rais Ruto kwa kutotekeleza miradi ya maendeleo aliyowaahidi wakazi wa Kakamega kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Rais Ruto, nataka kukuambia kwamba umetenga jamii ya Waluhya kimaendeleo. Umefeli kutekeleza ahadi ulizotoa kwa watu wetu na umekuwa ukituambia kile unapania kufanya. Msimu wa uhadi uliishi, huu ni wakati wa kutekeleza,” akaeleza Dkt Khalwale huku akimlaumu Dkt Ruto kwa kutekeleza miradi mikubwa Luo Nyanza ambako wakazi hawakumpigia kura 2022.