Habari

Msanii Betty Bayo afariki akitibiwa saratani

Na BENSON MATHEKA November 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TASNIA ya muziki wa injili nchini inaomboleza kifo cha msanii mashuhuri Betty Bayo, ambaye alifariki dunia Jumatatu Novemba 10, 2025 baada ya kuugua saratani ya damu.

Kifo chake kilithibitishwa na Mhubiri Victor Kanyari, aliyekuwa mumewe na baba wa watoto wao wawili, ambaye aliongoza familia yake na marafiki katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ambapo marehemu alikuwa akipokea matibabu.

Kanyari aliambia Taifa Dijitali kwamba Betty alikuwa amelazwa hospitalini humo kwa wiki moja kabla ya kufariki jana.

“Betty alikuwa hospitalini kwa wiki moja. Alifariki Novemba 10, 2025 saa kumi na moja asubuhi,” alisema.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa mitandao ya kijamii, Askofu Kanyari alimuomboleza mkewe huyo wa zamani.

“Inauma kwa njia siwezi kueleza. Umeondoka kabla sijakueleza yote niliyotaka. Nakusikia bado katika kicheko cha watoto wetu na kila tabia ndogo inayanikumbusha wewe. Tulipitia mengi, lakini kupitia yote, ulikuwa familia. Nitabeba kumbukumbu zako, upendo wako na roho yako daima. Pumzika salama, utakumbukwa milele.”

Marafiki wengi kutoka sekta ya muziki na viongozi wa kidini walimuomboleza kupitia mitandao ya kijamii.

“Ameacha urithi wa mchango mkubwa katika ukuaji wa muziki wa injili, urafiki, na moyo wa kujitolea. Alihudumu na sasa amepumzika.. Pumzika kwa amani Betty Bayo, hata saratani itakufa siku moja,” alisema Askofu Benson Kamau.

Mwanahabari wa Inooro TV, Wakarura Wa Nyutu, naye alieleza huzuni yake, akifichua kuwa alikutana na Bayo mara ya mwisho Jumatatu, Novemba 3.

“Wiki iliyopita nilikuwa nyumbani kwako. Tulikaa hadi karibu saa sita usiku tukicheka na kuzungumza, nikiamini utapona. Sasa umetuacha,” aliandika.

Betty Bayo alipata umaarufu kupitia nyimbo zake maarufu “Eleventh Hour” Maneno, Atasimama Nawe, Ngai ti Mundu, Kuhandwo na Siyabonga zilizogusa nyoyo za mashabiki wengi kwa ujumbe wake wa matumaini na imani.

Dalili za kuzorota kwa afya yake zilianza kuonekana Agosti 2025, alipochapisha picha akiwa hospitalini akipumua kwa msaada wa oksijeni.