Mnajisi kutafunwa na chawa jela miaka 20
MAHAKAMA ya Siaya imemhukumu mwanaume mmoja kifungo cha miaka 20 jela baada ya kumpata na hatia ya kumnajisi mtoto.
Kevin Ondif alianza kutumikia kifungo chake baada ya Hakimu wa Siaya, Jacob Mkala, kushawishiwa na hoja za upande wa mashtaka ambao uliwasilishwa na mashahidi watano.
Hukumu iliyosomwa mahakamani ilisema, “Serikali imeweza kuthibitisha kuwa mlalamishi alikuwa mtoto wakati wa tukio na kuwa ni mshtakiwa aliyevunja heshima ya mlalamishi. Mshtakiwa alimnajisi kwa nguvu na kumfanya apate majeraha makubwa sehemu za siri na kihisia.”
Hakimu Mkala aliongeza katika hukumu yake kwamba “Mwisho, napata kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi yao bila shaka yoyote. Kwa hivyo, mshtakiwa amepatikana na hatia na atahukumiwa chini ya kifungu cha 215 cha Sheria ya kesi za uhalifu.”
Mahakama iliambiwa kuwa Januari 1, 2021, katika kijiji cha Nyamawanga B, eneo dogo la Bar Osimbo, Kaunti ya Siaya, mshtakiwa Ondif, akiwa na wanaume wengine watano, walimkabili mlalamishi njiani alipokuwa akitoka kwenye saluni na kumpeleka kwenye nyumba fulani ambapo alifungiwa ndani.
Mlalamishi alikuwa na umri wa miaka 14 wakati wa tukio hilo.
“Nilienda sokoni siku hiyo kusukwa nywele. Njiani, nilinizuia na wanaume watano ambao sikuwajua. Walitumia kisu kidogo cha mkononi na kutisha kuniua ikiwa ningepiga kelele,” mlalamishi aliambia mahakama.
Aliongeza, “Pamoja walinipeleka kwenye boma fulani ambapo walinifungia ndani ya moja ya nyumba tatu zilizokuwa hapo. Mara tu nilipofungiwa, wanaume wanne waliondoka, na kuacha mmoja ndani ya nyumba hiyo.”
Alidai pia kuwa mshtakiwa alimlazimisha kufanya tendo la ngono bila kinga kutoka jioni hadi usiku wa manane.
“Katikati ya usiku, mwanaume mwingine alikuja na kufungua mlango. Mshtakiwa wangu aliwasha msumaa, mwanaume huyo alimuita Kevin na naye akajibu. Ndipo niligundua kuwa jina lake ni Kevin. Alitoka nje na kuzungumza na mwanaume huyo,” aliambia mahakama ya Siaya.
Aliporudi ndani ya nyumba, Kevin alimwambia mlalamishi kuwa alitaka kwenda kutembea na kwamba alipaswa kuondoka nyumba yake.
“Alinifukuza nje ya nyumba na kuniacha kando ya barabara nikaenda nyumbani,” alisimulia mlalamishi.
Mlalamishi aliripoti kitendo hicho kwa mama yake ambaye alimpeleka hospitali na baadaye akapiga ripoti katika kituo cha polisi cha Barogongo.
Mahakama pia ilisikia kuwa baada ya kuripoti kwa polisi, mlalamishi aliwapeleka maafisa hadi nyumba ambapo alitendewa kitendo hicho na wakamkuta mshtakiwa akifua nguo; mlalamishi alisema kuwa mshtakiwa bado alikuwa amevaa nguo alizokuwa amevaa wakati wa kumnajisi.
Afisa wa uchunguzi, Hosea Kipkoech, alithibitisha mahakamani kuwa baada ya kuripoti, mlalamishi aliwapeleka kwenye eneo la tukio na kutambua nyumba aliyofungiwa ndani.
Hakimu Mkala pia aliambiwa kuwa mshtakiwa alitoweka kwa karibu miaka miwili baada ya kugundua kuwa alikuwa akisakwa ba polisi.
Alikamatwa Desemba 29, 2023 baada ya kurudi nyumbani.