Mimi si mkaidi-Katibu asema akifika mbele ya kamati ‘aliyokaidi’ mara 16
BAADA ya kukosa kufika mbele ya wabunge mara 16, Katibu wa Wizara ya Fedha Dkt Chris Kiptoo hatimaye alijitokeza mbele ya Kamati Maalum ya Uhasibu wa Fedha za Umma kujibu maswali kuhusu matumizi ya fedha katika hazina 14 chini ya usimamizi wake.
Dkt Kiptoo aliomba radhi kwa kutofika mara zilizopita, akisema majukumu yake katika Wizara ya Fedha humfanya kuwa “ katibu mwenye kazi nyingi zaidi serikalini.”
“Ni bahati mbaya sana kwamba imechukuliwa kwamba nilikaidi kufika mbele ya kamati hii. Nina hakika nitafika mtakaponihitaji, lakini pia muelewe, kazi yangu ni nzito sana. Mimi ndiye katibu mwenye shughuli nyingi zaidi,” alisema Dkt Kiptoo.
Kauli hiyo haikuwafurahisha wabunge, ambao walimlaumu kwa kupuuza kamati hiyo huku akiendelea kuhudhuria vikao vya kamati nyingine kama ile ya Fedha na Mipango ya Taifa.
“Unasema wewe ni una kazi nyingi lakini unafika mbele ya kamati nyingine, basi unaidharau kamati hii,” alisema Mwenyekiti wa kikao hicho, Mbunge wa Imenti Kaskazini Rahim Dawood.
Bw Dawood aliongeza: “Kwa zaidi ya miaka miwili na nusu hujawahi kufika. Labda tumuombe Rais aondoe baadhi ya hazina hizi kutoka kwako kwa sababu unaonekana hauna muda wa kuzisimamia ipasavyo.”
Mwakilishi wa Wanawake wa Busia, Catherine Omanyo, alimshauri Dkt Kiptoo kugawa majukumu ili kupunguza mzigo wa kazi.
“Sijaona uso wako kwa miaka mingi. Nilijiuliza, huyu mtu ni maalum kiasi gani? Wewe si Mkenya pekee unayeweza kufanya kila kitu. Usijaribu kujionyesha kama unafanya kazi kupita kiasi,” alisema.
Bw Dawood aliongeza kuwa katibu huyo amekuwa akiitikia mara moja wito wa Kamati ya Fedha lakini si wa kamati yake.
“Unapoitwa na Kamati ya Fedha unakimbia, basi fanya vivyo hivyo tukikuita sisi,” alisema kwa ukali.
Mbunge wa Mbooni, Erastus Kivasu, alisema kutofika kwa katibu kumechelewesha ripoti ya kamati hiyo kuhusu usimamizi wa fedha.
“Kamati hii bado haijamaliza kazi kwa sababu katibu amekuwa akikosa kufika. Je, unaweza kutuhakikishia kuwa ukikosa leo, utafuja tutakapokuita tena?” aliuliza.
Dkt Kiptoo, kwa upande wake, alilalamika kuhusu vyombo vya habari, akisema vimeeneza taarifa za uongo.
“Nilisoma Taifa Leo wakiandika ‘Mkubwa Mkaidi’ na nikajiuliza huyo mkubwa ni nani? Mimi nimekuwa nikifika kila ninapoitwa,” alisema.
Hata hivyo, Bw Kivasu alimkosoa vikali akisema: “Vyombo vya habari vilisema ukweli. Tuna barua tulizokutumia mara kadhaa, na ushahidi wote uko hapa.”
Kikao hicho kiliendelea baada ya Dkt Kiptoo kuahidi kuwa atahudhuria vikao vyote vijavyo atakapoitwa.