Habari

Kenya sasa kufungua ubalozi Vatican

Na STEVE OTIENO November 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KENYA sasa inalenga kufungua ubalozi mpya katika Jiji la Vatican kufuatia idhini ya Baraza la Mawaziri Novemba 11, 2025.

Hii inaonekana kama hatua kubwa inayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hiyo na Makao Makuu ya Kanisa Katoliki.

Katika kikao kilichofanyika Ikulu ya Nairobi, Baraza la Mawaziri lilisema ubalozi huo mpya utaimarisha uhusiano wa pande mbili kati ya Kenya na Vatican, kukuza ushirikiano katika ujenzi wa amani, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kuendeleza kazi za kibinadamu.

Pia utafungua njia za ushirikiano na taasisi mbalimbali za kidini zinazoendeshwa na Vatican kote duniani.

Vatican City, ambayo ndiyo makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani, ina jukumu muhimu katika mazungumzo ya kimataifa na shughuli za maendeleo kupitia ushawishi wake wa kidiplomasia, kibinadamu na wa kidini.

Baraza hilo lilibaini kuwa ubalozi wa kudumu mjini Vatican utakuwa jukwaa muhimu kwa Kenya kutumia mtandao mkubwa wa Kanisa Katoliki katika miradi ya kijamii na ya maendeleo, hususan kwenye sekta za elimu, afya, na kupunguza umaskini.

“Kufunguliwa kwa ubalozi huo kutaimarisha ushirikiano wetu na mashirika ya maendeleo ya Kanisa Katoliki yanayoendesha zaidi ya shule 7,700 na vituo vya afya 500 nchini Kenya,” ilisema sehemu ya taarifa ya Baraza la Mawaziri.

Uamuzi huo pia unaonyesha Kenya inathamini jukumu la Vatican katika kukuza amani, haki za kijamii na haki za binadamu, maeneo ambayo Kanisa Katoliki limekuwa mshirika muhimu katika safari ya maendeleo ya taifa.

Mbali na Vatican, Baraza la Mawaziri pia limeidhinisha kufunguliwa kwa balozi mbili mpya mjini Copenhagen (Denmark) na Hanoi (Vietnam). Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Kenya wa kupanua ushawishi wake wa kidiplomasia na kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kitamaduni na kimaendeleo na nchi washirika duniani.

Ubalozi wa Copenhagen unatarajiwa kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa maendeleo kati ya Kenya na Denmark, na kufungua fursa mpya za ushirikiano katika kawi safi, ustahimilivu wa tabianchi, na teknolojia.