Ukimtaka Kalonzo, enda Wamunyoro uongee na Riggy G, Eugene amwambia Ruto
KIONGOZI wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K), Eugene Wamalwa, ametangaza kuwa msemaji rasmi wa Umoja wa Upinzani ni Rigathi Gachagua.
Huku akionekana kurejelea ufichuzi wa Rais William Ruto kwamba anajizatiti kumvutia kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka upande wake, Bw Wamalwa alisisitiza kuwa mazungumzo yoyote na kinara yeyote wa upinzani sharti yafanywe kupitia Bw Gachagua.
“Familia ya Umoja wa Upinzani iko na msemaji mmoja ambaye ni binamu yetu, Rigathi Gachagua,” akasema Bw Wamalwa Novemba 12, 2025 kwenye ujumbe kupitia akaunti yake ya mtandao wa X, huku akikariri kujitolea kwa vinara hao kudumisha umoja.
“Ikiwa mtu yeyote anataka kufikia upinzani anajue wa kumfikia; aende Wamunyoro akazungumze naye. Umoja wetu sharti udumishwe, ndio silaha kali zaidi ya upinzani,” akaongeza.
Kauli Bw Wamalwa, ambaye ni Waziri wa zamani wa Ulinzi, imejiri wakati ambapo Rais Ruto ameratibiwa kufanya ziara rasmi ya siku nne katika eneo pana la Ukambani.
Ziara yake itaanza Jumatano, Novemba 12, 2025 katika Kaunti ya Makueni ambapo ametaribiwa kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo ambapo anatarajiwa kuwarai viongozi wa eneo hilo, akiwemo Musyoka, kuiunga mkono serikali yake.
Aidha, onyo la Wamalwa limejiri wiki chache baada ya Gachagua kujitangaza kuwa msemaji rasmi wa Umoja wa Upinzani.
Akiongea mwezi Oktoba, Gachagua alimshambulia Rais Ruto akimwonya dhidi ya kuendesha kampeni za kumtaka Bw Musyoka kugura upinzani na kujiunga na mrengo wa Kenya Kwanza.
“Wewe Ruto koma kabisa kuwatuma watu kumtafuta Kalonzo, ukimtaka kuja uongee na mimi moja kwa moja,” Bw Gachagua alisema akiwa Murang’a alipohudhuria tamasha ya ngoma ya kitamaduni iliyoandaliwa na Kundi la Mawakili kutoka Mlima Kenya.
Mnamo Septemba 20, 2025, Bw Musyoka pia alimtaka Rais Ruto kukoma kuwatuma viongozi wa kidini kutoka Ukambani kumshawishi alijiunge na serikali akisema juhudi hizo hazitazaa matunda.
“Mniruhusu nimjibu Rais leo. Sharti nimjibu. Aliwatuma viongozi wa kidini kuja kuongea na viongozi wa Ukambani, akiwemo mimi, akitaka tufanye kazi na serikali yake ndipo serikali ilete maendeleo katika eneo la Ukamba. Ningependa kuwaambia viongozi wa kidini wakome kuingia kwenye mtego wa William Ruto, wakatae kibarua cha kunishawishi nijiunge naye. Ni haki ya kikatiba kwa wakazi wa Ukambani kupata maendeleo lakini wawe serikalini au la,” akasema Bw Musyoka akiwa katika Kanisa la Calvary Christian Tabernacle mjini Machakos.