Habari

Watoto 44,000 wanaoishi katika makao ya watoto kuunganishwa na familia zao 2032

Na COLLINS OMULO November 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WATOTO 44,000 wanaoishi katika makao ya kibinafsi ya watoto mayatima na wale wanaoishi katika taasisi nchini watarudishwa kwa familia zao kufikia mwaka 2032.

Kwa mujibu wa Wizara ya Jinsia na Huduma za Watoto, mchakato huo tayari umeanza na utafanyika hatua kwa hatua huku serikali ikifuatilia maendeleo ya watoto ambao tayari wameunganishwa na familia zao.

Akizungumza mbele ya Seneti Novemba 12, 2025, Waziri wa Jinsia na Huduma za Watoto Bi Hanna Cheptumo alisema zoezi hilo linatekelezwa kwa awamu hadi pale watoto wote walio katika taasisi watakapounganishwa kikamilifu na jamii.

“Tuna mkakati kupitia mageuzi ya kitaifa ya malezi kuhakikisha watoto wote wanahamishiwa kwa familia zao kufikia mwaka 2032. Hata hivyo, tunafanya hivyo kwa utaratibu kwa sababu hatuwezi kuwarudisha watoto kwenye mazingira ambayo hayajakaguliwa ipasavyo,” alisema Bi Cheptumo.

“Tunahakikisha mchakato unafanywa kwa uangalifu ili kuepuka matukio ya ukatili au unyanyasaji wa watoto, hasa kutoka kwa watu ambao hawajazoea kuishi nao kwa muda mrefu,” aliongeza.

Alikuwa akijibu swali la Seneta Mteule George Mbugua, ambaye alitaka kujua hatua iliyochukuliwa katika mpango wa serikali wa kufunga makao ya watoto na kuanzisha mfumo wa malezi wa kijamii na kifamilia.

Mwaka huu, serikali ilitangaza kuwa itafunga makao yote ya kibinafsi ya watoto nchini, ikiwa ni sehemu ya mageuzi ya mfumo wa malezi kupitia Baraza la Kitaifa la Huduma za Watoto, ili kuimarisha malezi ya kifamilia na kijamii.

Kulingana na takwimu za hivi karibuni za serikali, kuna taasisi 902 za watoto za hisani zilizo na takribani watoto 44,070, na taasisi 30 za serikali zilizo na  watoto 1,443.

Seneta Mteule Esther Okenyuri alitaka kujua mikakati iliyowekwa na serikali kuhakikisha watoto wa mitaani wanasaidiwa au kuunganishwa na familia zao.

“Kuna ongezeko la watoto wanaoishi mitaani, hasa Nairobi, ambapo wengine wanahusishwa na ajira za utotoni. Serikali inafanya nini kuwasaidia watoto hawa?” aliuliza.

Bi Cheptumo alisema serikali imekamilisha sensa ya watoto hao na matokeo ya awali yanaonyesha kuwa baadhi yao si Wakenya pekee, bali pia ni raia wa nchi jirani.

Alisema wizara itatumia ripoti hiyo kubaini watoto wanaoweza kuunganishwa na familia zao na wale wanaohitaji ukarabati au malezi maalum.