Makala

Jaji apiga marufuku mikaratusi karibu na mito, chemi chemi za maji

Na BENSON MATHEKA November 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Mahakama ya Mazingira na Ardhi  mjini Ol Kalou imepiga marufuku miti ya mikaratusi ndani ya umbali wa mita 30 kutoka kwa vyanzo vya maji na mita 10 kutoka mipakani.

Katika uamuzi wake, Jaji Mugo Kamau ameagiza Bunge la Kitaifa kutunga sheria zitakazodhibiti upanzi wa mikaratusi nchini ndani ya kipindi cha miezi 12.

Wakati sheria hizo zikitayarishwa, mahakama imetoa mwongozo wa muda wa kusimamia upanzi wa miti hiyo.
Miongoni mwa maagizo hayo ni kuondoa na kupiga marufuku upanzi wa mikaratusi iliyo chini ya mita 30 kutoka chemi chemi za maji, mito, mabwawa, mabonde ya maji, maziwa na bahari.

Aidha, miti hiyo haitaruhusiwa kupandwa katika maeneo ya mabwawa au mashamba yanayotumika kwa unyunyuzaji, kwenye ardhi  ya chini ya robo ekari, au katika maeneo yenye mvua chini ya milimita 400 kwa mwaka, isipokuwa kwa idhini maalum kutoka kwa Waziri wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi.

“Kwa kuepusha shaka, maagizo haya yatatekelezwa kote nchini, na washtakiwa wanaamrishwa kuhakikisha utekelezaji wa uamuzi huu,” alisema Jaji Mugo.

Amri hiyo ilitolewa kufuatia ombi lililowasilishwa na mwanaharakati wa mazingira na wakili Wilfred Omariba, ambaye alidai kuwa miti ya mikaratusi ndiyo chanzo cha kukauka kwa vyanzo vya maji nchini.

Katika kesi aliyowasilisha mwaka 2022, Bw Omariba alishtaki serikali kwa kushindwa kudhibiti upanzi kiholela wa mikaratusi, jambo alilosema limesababisha madhara makubwa kwa mazingira.

Akitaja mifano kutoka Kaunti za Kisii na Nyamira, wakili huyo alisema miti hiyo imepandwa karibu na chemchemi na maeneo ya  maji, na hivyo kupunguza kiasi cha maji katika mito na mabwawa.
Alisema kwa zaidi ya miaka 40, serikali imepuuza tatizo hilo na kushindwa kuweka sheria za kulinda mazingira.

“Kiasi cha maji kimepungua kiasi kwamba wananchi sasa wanagombania maji na serikali imelazimika kuchimba visima,” alisema. “Zamani watu wa Kisii na Nyamira walijitosheleza kwa chakula, sasa wananunua kutoka kaunti nyingine, mikaratusi ndiyo sababu.”

Alionya kuwa ikiwa hali itaendelea, kaunti zenye maeneo ya maji zinaweza kutoweka ndani ya miaka 50 ijayo, na Kenya inaweza kugeuka jangwa.

Alishtaki Waziri wa Mazingira, Waziri wa Maji, NEMA, Huduma za Misitu Kenya (KFS) na  Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mahakama ilipatia serikali siku 45 kabla ya kuanza kutekeleza agizo hilo.

Baada ya hukumu, Bw Omariba alielezea furaha yake, akisema uamuzi huo ni ushindi kwa wananchi, mazingira na vizazi vijavyo.