Kanja: Kuzima usajili wa makurutu ni kuhatarisha usalama wa nchi
INSPEKTA Jenerali wa Polisi Douglas Kanja ameiomba Mahakama Kuu kuondoa kwa dharura agizo lililositisha usajili wa makurutu wa polisi 10,000, akionya kuwa uhaba wa maafisa ni tishio kwa usalama wa nchi.
Kupitia hati zake mahakamani, Kanja anadai kuwa kusitishwa kwa zoezi hilo kulitokana na taarifa zisizo kamili zilizowasilishwa na mlalamishi Eliud Matindi, aliyepinga uhalali wa zoezi la usajili huo.
Mvutano huu wa kisheria unatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu wa Novemba 10, 2025, uliosimamisha zoezi la usajili baada ya kesi kuwasilishwa na Matindi.
Hata hivyo, Kanja sasa anamshutumu Matindi kwa kuficha ukweli muhimu kuhusu uamuzi wa hivi karibuni wa Mahakama ya Kazi na Ajira, ambao ulithibitisha kwamba jukumu la kuajiri maafisa wa polisi ni la Inspekta Jenerali chini ya Kifungu cha 245(4)(c) cha Katiba, na sio la Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC).
“Kesi hii iliwasilishwa bila mahakama kuarifiwa kuwa mzozo huo huo uliamuliwa kikamilifu wiki tatu zilizopita,” linasema ombi la Bw Kanja, akionya kuwa kusitishwa kunaweza kudhoofisha shughuli za usalama katika kipindi hiki cha ongezeko la uhalifu. Kesi iliwasilishwa katika Mahakama ya Katiba, Milimani, chini ya ombi la dharura.
Serikali imeonya kuwa Kenya inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maafisa wa polisi kufuatia marufuku ya miaka mitatu ya uajiri, hali iliyoathiriwa zaidi na kustaafu na kujiuzulu kwa askari wengi.
Kanja alisema kuwa kusimamishwa kwa usajili wa makurutu ambao maandalizi yake yalikuwa yamekamilika, kutaiweka nchi katika hatari kubwa ya kiusalama.
“Uchaguzi unahitaji idadi kubwa ya askari kwa ajili ya usalama. Tunahitaji muda wa kutosha kuwafunza kabla ya kuwatuma kazini,” alisema, akiongeza kuwa changamoto za usalama nchini zimekuwa zikiongezeka kutokana na uhaba wa maafisa wa kutosha.
“Kuchelewesha au kusimamisha uajiri huu kutanyima Huduma ya Polisi muda wa kutosha kuwafunza na kuwatuma askari katika majukumu ya kiusalama,” alionya.