Mbunge wa Isiolo Kusini Tubi Bidu afariki dunia
MBUNGE wa Isiolo Kusini, Tubi Bidu Mohamed, ameaga dunia Jumatano, Novemba 12, 2025, akipokea matibabu katika hospitali ya Nairobi.
Akitoa tangazo kuhusu kifo hicho, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alisema kuwa mbunge huyo wa chama wa Jubilee alikufa majira ya jioni.
Mheshimiwa Tubi Bidu alikuwa anahudumu muhula wake wa kwanza bungeni baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2022.
“Kwa huzuni kuu, ninawatangazia na taifa kwa ujumla kifo cha mwenzetu Mbunge wa Isiolo Kusini Mheshimiwa Tubi Bidu Mohamed aliyetuacha jioni hii, Jumatano Novemba 12, 2025, akipokea matibabu Nairobi Hospital,” akaeleza.
Hadi kifo chake, mwendazake, alihudumu kama mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Mazingira, Misitu na Madini na Kamati ya Kushughulikia Malalamishi ya Umma.
Kabla ya kuchaguliwa kwake, Mheshimiwa Tubi Bidu alihudumu kama Spika wa Bunge la Kaunti ya Isiolo kuanzia 2013 hadi 2017.
“Waheshimiwa wabunge, tunapoomboleza tumkumbuke Mheshimiwa Tubi kwa mchango wake uliofaidi taifa hili. Tunaombea familia, marafiki, wakazi wa Isiolo Kusini na wale wote waliomfahamu. Roho yake ipumzike pema penye amani,” Bw Wetang’ula akaeleza.