Michezo

Ronaldo kustaafu baada ya Kombe la Dunia

Na JOHN ASHIHUNDU Na MASHIRIKA November 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MSHINDI mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or, Cristiano Ronaldo amesema atastaafu kuchezea timu ya taifa ya Ureno mwaka ujao baada ya Kombe la Dunia.

Mchezaji huyo hodari pia alisema kuwa atastaafu rasmi kusakata soka ndani ya kipindi cha mwaka mmoja au miwili ijayo.

Hata hivyo, Ureno haijafuzu kwa kipute hicho kitakachofanyika nchini Amerika, Canada na Mexico kwa wakati mmoja, lakini inaweza kujihakikishia nafasi hiyo ikiwa itaibuka na ushindi dhidi ya timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland ugenini leo usiku ugani Aviva Dublin

Hii itakuwa mara ya sita kwa supastaa huyo wa klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia kuchezea Ureno kwenye Kombe la Dunia. Mara ya kwanza ilikuwa 2006, akiwa na umri wa miaka 21.

Mshambuliaji huyo matata mwenye umri wa miaka 40 aliweka rekodi ya kufikisha zaidi ya mabao 950 katika ngazi ya klabu na kimataifa.

Akiwa na timu ya taifa, Ronaldo alishinda taji lake la tatu kwa kuishinda Uhispania kwa 5-2 kwenye fainali ya Ligi ya Kombe la Mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League) kupitia kwa mikwaju ya peanlti ugani Allianz Arena nchini Ujerumani baada ya mechi kumalizika kwa sare ya 2-2 hata baada ya muda wa nyongeza wa dakika ya 120.

Kufikia sasa, Ronaldo ameonekana kutokuwa na uhakika wa maisha yake ya baadye kwenye klabu ya Al-Nassr wakati mkataba wake unakaribia kufika kikomo mwishoni mwa msimu huu tangu ajiunge na klabu hiyo ya Saudi Pro League mnamo 2023 kwa misimu miwili.

Licha ya Ireland kuwa wenyeji wa pambano la leo, Ureno wanapewa nafasi kubwa ya kupata ushindi kutokana na uzoefu wa kikosi hicho cha kocha Roberto Martinez ambacho hakijashindwa katika mechi tano zilizopita, kukijifunia ushindi mara nne na sare moja.

Isitoshe, Ireland wanajivunia ushindi mmoja tu katika mechi zao kumi, licha ya sare ya majuzi ya 2-2 dhidi ya Hungary ugani Etadio Jose Alvalade, ambako Christiano alifunga mabao mawili kabla ya Hungary kutoka nyuma na kusawazisha mechi ikielekea kumalizika.

Ureno wanaendelea kuongoza Kundi F, wakihitaji tu ushindi mmoja katika mechi zao mbili zilizobakia. Baada ya kucheza na Ireland ugenini leo, Jumapili kikosi hicho cha Martinez takakuwa nyumbani kualika Armenia wanaoshikilia mkia kwenye kundi hilo.

Ratiba ya mechi za leo: Uingereza vs Serbia (10:45pm), Ufaransa vs Ukraine (10:45pm), Armenia vs Hungary (8pm), Azerbaijan vs Iceland (8pm), Norway vs Estonia (8pm), Moldova vs Italia (10:45pm), Andorra vs Albania (10:45pm), Jamhuri ya Ireland vs Ureno (10:45pm), Czechia vs San Marino (8pm), Lithuania vs Israel (8pm), Macedonia Kasakzini vs Latvia (8pm).