Afya na Jamii

Madhara ya kichokonoo kwenye meno

Na WANGU KANURI November 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KILA wakati baada ya kula chakula, watu wengi hutumia kichokonoo (toothpick) kuondoa mabaki ya chakula katikati ya meno.

Hata hivyo, Dkt Serah Wanza, mtaalamu wa afya ya meno katika hospitali ya Versatile Dental Solutions, anaeleza kuwa matumizi mabaya ya kifaa hiki huenda yakaathiri ufizi.

Kati ya jino moja na jingine, kuanzia sehemu ambayo meno yanagusa mfupa kwenda chini, kuna nafasi ya pembetatu. Nafasi hii hujazwa na ufizi (interdental papilla).

“Ni kawaida kabisa kwa mabaki ya chakula kusukumwa kwenye nafasi hii wakati wa kutafuna. Ulimi na mashavu husogeza chakula, na wakati mwingine kinaweza kukwama hapo. Lakini hali hii huwa dhahiri zaidi kama nafasi hiyo iko wazi,” anaeleza.

Athari za kichokonoo

Tofauti kuu ya kichokonoo na uzi mwembamba unaotoa vyakula kwenye mswaki haufikii (dental floss), ni kwenye vifaa hivi vinaweza kufikia, anasema Dkt Wanza.

Kichokonoo huwa kinene, na mara nyingi husafisha juu juu tu kati ya meno.
“Ikiwa chakula kimeingia kidogo nyuma ya ufizi, kichokonoo hakiwezi kufika huko na unaweza kusukuma chakula zaidi kuelekea chini ya ufizi badala ya kukitoa.”

Kutumia utepe wa kuondoa mabaki ya chakula ndani ya meno (string floss) ni bora zaidi kuliko kutumia kichokonoo, kwa sababu kichokonoo kinaweza kusababisha ufizi kusongea nyuma.

Isitoshe, Dkt Wanza anasema kutumia kichokonoo kila siku huweka presha kwenye ufizi ambayo inaweza kuonekana au kuhusishwa kama haina madhara, lakini kujirudia huko kunadhuru ufizi, na baadaye kunaleta uvimbe kwenye ufizi kisha ufizi unaathirika zaidi.

Zaidi ya hayo, kutumia kichokonoo mara kwa mara asema kunaweza sababisha nafasi kati ya meno.

“Sio kwa sababu ya kichokonoa kusukuma na kutenganisha meno bali ni tishu za ufizi zinazosongea kutokana na majeraha na msuguano wa mara kwa mara. Hivyo ile nafasi ya pembetatu kati ya meno ambayo ilipaswa kujazwa na ufizi, inakuwa wazi na kuonekana kama sehemu nyeusi kati ya meno karibu na ufizi,” Dkt Wanza anaelezea.

Je, ni njia gani sahihi ya kutumia kichokonoo?

Iwapo mtu atalazimika kutumia kichokonoo, Dkt Wanza anashauri kutumia ukiwa mbele ya kioo, ili uweze kuona unachofanya.
Lengo ni kuwa mwangalifu bila kudunga ufizi.

“Ukitoa mabaki ya chakula kwenye meno yako, unapaswa kuhakikisha kuwa unatumia kichokonoo chako kwa upole ukisogeze sambamba na sehemu ya juu ya jino, si kushuka kwenda kwenye ufizi. Lengo ni kuinua chakula, sio kukisukuma chini,” anaeleza Dkt Wanza.

Je, vichokonoo vinaweza kusababisha maambukizi?

“Ndio vinaweza. Kwanza, iwapo havikufunganywa kwa kuzingatia usafi na pili, iwapo kipande kidogo cha kichokonoo hicho kimebaki katikati ya nafasi ya meno.”

Dkt Wanza anaeleza kuwa hii huwa hali kwa sababu mwili hukiona kama kitu kigeni na hufura kama njia ya kujilinda. Ikiwa hali hii haitashughulikiwa basi huenda ukapata maambukizi.

Zaidi ya matumizi bora ya kichokonoa, Dkt Wanza anasema kuwa manufaa halisi ya nyuzi nyembamba za kutoa mabaki ya chakula yanapatikana tu ukifanya kwa usahihi.

Njia mwafaka ni kuhakikisha kuwa uzi umelikumbatia jino kwa umbo la C. Hivyo uzi huo unaweza kufika chini ya ufizi, sehemu ambayo mabaki na bakteria hujikusanya.

“Ili kutoa mabaki hayo, songeza uzi huo juu na chini kwa kuzingatia umbo lile ili usafishe jino ipasavyo.”

Mbali na uzi wa kuondoa mabaki ya chakula, Dkt Wanza anasema unaweza kutumia kifaa cha kuondoa mabaki kwa kutumia maji (water flossers) haswa kwa watu ambao meno yao yamejazana kwa sababu wana ufizi mdogo.

“Pia kuna mswaki mdogo unaotumiwa kusafisha meno pale ambapo mswaki wa kawaida haufikii (interdental brushes).”

Lakini, Dkt Wanza anaeleza kuwa hapendekezi matumizi ya mswaki huu kwa watu wenye nafasi ndogo kati ya meno, kwani wanaweza wakaumiza ufizi.

Hata hivyo, changamoto kubwa katika matumizi ya kutumia uzi kuondoa mabaki ya chakula ni kutofuata njia iliyoelezwa hapo juu. Dkt Wanza anapendekeza matumizi ya uzi huu kuondoa mabaki ya chakula angalau mara moja kwa siku angalau jioni.