Maoni

Wanaokiuka haki za watoto waadhibiwe vikali kisheria

Na MARY WANGARI November 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANAFUNZI wa Gredi ya 9 majuzi alipatikana akiwa ameuawa kinyama na mwili wake kutupwa katika shamba la miwa Kaunti ya Narok.

Mtoto huyo alikuwa akielekea shuleni kushiriki mitihani ya kitaifa ya KJSEA, na washambulizi waliomtendea unyama na kukatiza maisha yake kikatili katika kisa kilichotikisa jamii eneo hilo na taifa kwa jumla.

Kisa hiki ni moja kati ya visa vinavyozua hofu kuhusu usalama na mustakabali wa kizazi kichanga huku ripoti zikifichua ongezeko la maovu dhidi ya watoto wasio na hatia ambao kosa lao tu ni kuzaliwa katika jamii katili isiyowajali.

Visa vya kuatua moyo vimekithiri kuhusu watoto wachanga wenye umri wa hadi miaka mitatu kuanzia kudhulumiwa kingono, kimwili na kisaikolojia, kunyimwa mahitaji ya kimsingi, haki zao kikatiba kukiukwa hadi kuuawa kiholela.

Katika miezi michache iliyopita, ripoti za kusikitisha zimeangazia jinsi watoto walivyobakwa, kulawitiwa, kuuawa na kuzikwa kikatili na watu walioaminiwa kuwatunza wakiwemo wazazi wao wenyewe, jamaa, majirani, marafiki, walimu na viongozi wa kidini, na katika mazingira yaliyodhaniwa kuwa salama kwa watoto mathalan nyumbani, shuleni na hata kanisani!

Huku shinikizo za kijamii, matatizo ya afya ya kiakili na gharama ya maisha ikizidi kuongezeka, watoto ndio wahasiriwa wakuu wa ukatili wa watu wazima hususan kwenye mafarakano ya kifamilia na ghasia za kisiasa.

Visa vingi vinavyohusu maovu dhidi ya watoto vingali havijasuluhishwa kutokana na mifumo duni, ukosefu wa sheria thabiti na mila potovu zinazopatia kipaumbele kudumisha usiri huku watoto wakiathirika.

Hali kwamba wahusika wanaweza kukwepa adhabu kirahisi, imezidi kuwapa ujasiri wanaowadhulumu watoto.

Mageuzi ya sheria yanahitajika kwa dharura ili kuwaadhibu vikali wahusika na kuwa onyo kwa wanaopanga kuwadhulumu watoto kwa namna yoyote.

Katika utamaduni wa Kiafrika uliorithishwa kutoka kizazi hadi kingine, mtoto alimilikiwa na jamii zima iliyoshirikiana kumtunza, kumlinda na kumnyoosha hadi alipokuwa mtu mzima anayeweza kutegemewa.

Kama taifa, tuna wajibu wa kuwalinda watoto na kuwahakikishia mazingira salama ya kufurahia utoto wao, kukua na kukomaa bila hofu.

Ni kinaya kupigania maendeleo ilhali tunaangamiza kizazi ambacho ndicho mustakabali wa jamii na taifa kwa jumla.

Ufanisi wa taifa hudhihirika kupitia jinsi wasio na uwezo wa kujitetea au kujipigania, wanavyotunzwa katika jamii.