Daktari asema Kalombotole hapaswi kujibu kesi ya mauaji
MTAALAM wa kibinafsi wa tiba ya akili aliyempima Kennedy Kalombotole anayeshtakiwa kuua mgonjwa katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) amesema akili yake sio timamu na hawezi jibu mashtaka ya mauaji.
Hata hivyo Jaji Diana Kavedza anayesikiza kesi dhidi ya Kalombotole aliamuru mshtakiwa asalie gerezani hadi ripoti ya tatu kuhusu utimamu wa akili yake itolewe na madaktari wa tiba wa KNH.
Jaji Kavedza aliamuru idara ya magereza impeleke Kalombotole KNH kupimwa utimamu wa akili yake kabla ya kusomewa shtaka la kumuua Gilbert Kinyua Muthoni mnamo Julai 17 2025.
Kinyua aliyekuwa na umri wa miaka 54 alikuwa amelazwa katika KNH Ward 7B alipopatwa na maafa.
Jaji Kavedza alisema endapo madaktari wa KNH watatofautiana na ripoti ya Dkt Fredrick Owiti itabidi aamuru jopo la madaktari wanne katika hospitali ya Mathari ibuniwe kumpima Kalombotole kabla ya hatma ya mshtakiwa kuamuliwa.
“Iwapo madaktari wa KNH watatofautiana na Dkt Owiti sitakuwa na budi ila kuamuru jopo la madaktari wanne katika hospitali ya Mathari kumpima Kalombotole na watoe ripoti yao kuhusu utimamu wa akili yake,” Jaji Kavedza alisema.
Mnamo Oktoba 23,2025 Jaji huyo aliruhusu mawakili wa mshtakiwa Joshua Ombegi, Zephamia Achapa na Philip Maiyo kumpeleka daktari wa kibinafsi kumpima mshtakiwa na kutoa ripoti ikiwa atashtakiwa au la.
Bw Ombegi alieleza mahakama Dkt Owiti alimpima mshtakiwa na kufikia uamuzi kwamba “hafai kufunguliwa mashtakiwa ya mauaji kwa vile akili yake sio timamu.”
Wakili huyo alisema ripoti ya Dkt Owiti imewasilishwa kortini na nakala nyingine kupewa kiongozi wa mashtaka.
Mahakama iliamuru kesi hiyo iahirishwe hadi Desemba 17,2025 ripoti ya KNH kuwasilishwa.
Awali mawakili wa familia ya mhasiriwa na wale wanaomtetea mshtakiwa walitofautiana ikiwa madaktari wa KNH watatoa ripoti sahihi ikitiliwa maanani mshtakiwa anadaiwa aliua wagonjwa mle.
Mahakama iliwaeleza mawakili kwamba KNH ni mojawapo ya hospitali kuu nchini zilizo na wataalam waliobombea na kamwe hawatakuwa na upendeleo wakimshughulikia mshtakiwa.
Jaji Kavedza aliwashauri mawakili waheshimu taaluma za watu wengine badala ya kuwashuku.
Kalombotole ataendelea kukaa katika gereza la eneo la viwandani hadi Desemba 17,2025 atakaporudishwa kortini KNH iwasilishe ripoti kuhusu utimamu wa akili yake.