Michezo

Afisa kutoka Shirikisho la Raga Duniani kuhudhuria Kombe la Afrika Nairobi

Na GEOFFREY ANENE November 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MKUU wa Mashindano, Utendaji na Maendeleo wa Shirikisho la Dunia la Raga (World Rugby), Nigel Cass, ameratibiwa kuwasili nchini Kenya Novemba 15, 2025 kabla ya Kombe la Afrika la raga itakalochezwa katika uwanjani RFUEA jijini Nairobi.

Ziara yake inaashiria kuongezeka kwa imani ya kimataifa kuhusu maendeleo ya mchezo wa raga nchini Kenya na inafuata ombi la Kenya kuwa mwenyeji wa raundi moja ya mashindano ya dunia ya daraja la pili ya HSBC Sevens Series.

Rais wa Shirikisho la Raga barani Afrika (Rugby Africa), Herbert Mensah, alisifu maendeleo makubwa ya Kenya katika mchezo wa wanawake, akitoa mfano wa ushindi maarufu wa Lionesses dhidi ya Afrika Kusini mapema mwaka huu.

“Kenya ina vipaji vya kipekee,” alisema wakati wa kuzinduliwa kwa Kombe la Afrika ugani RFUEA, Alhamisi. “Tunataka kushirikiana na serikali na Shirikisho la Raga Kenya (KRU) kuhakikisha uwekezaji unaendelea. Tukidumisha ushirikiano huu, Rugby Africa itawezesha Kenya kuwa mwenyeji wa angalau mashindano mawili au matatu makubwa, na huenda hata tukaleta mashindano ya HSBC hapa,” akasema raia huyo wa Ghana.

Mensah, ambaye pia ni mwanachama wa bodi ya World Rugby, alisema mazungumzo yake na Waziri wa Michezo Salim Mvurya yatakuwa juu ya nafasi ya Kenya kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa duniani. “Tuna imani na uongozi wa Kenya na serikali yake. Kwa maoni yangu, ukuu wa Kenya unatokana na raga,” alisema, akiongeza kuwa mashindano yajayo yatakuwa ya kwanza duniani ambapo waamuzi, maafisa wa mechi na waandaaji wote watakuwa wanawake.

Kutoka kushoto hadi kulia: Nahodha wa Kenya Lionesses Sheila Chajira (aliye na mpira), Waziri wa Michezo Salim Mvurya, na manahodha wa zamani Grace Okulu na Janet Okello wafurahia wakati wa uzunduzi wa Kombe la Afrika la raga ya wachezaji saba kila upande la wanawake mnamo Novemba 13, 2025. PICHA|GEOFFREY ANENE

Kwa upande wake, Mvurya alielezea mashindano hayo kuwa ya kihistoria na kielelezo cha ukuaji wa michezo nchini. “Hii ni siku spesheli sana. Timu yetu ya Lionesses imekuwa ikifanya vizuri, na nawaalika Wakenya wote waje kuwashangilia wanapopambana kushinda,” akasema. “Mashindano haya ya Afrika yanaimarisha nafasi ya Kenya kama nguvu ya bara katika mchezo wa raga.”

Alisisitiza dhamira ya serikali kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya michezo, akitaja karibu kukamilika kwa uwanja mpya wa Talanta unabeba mashabiki 60,000, utakaotumika kwa mashindano ya kimataifa yajayo. Aidha, alithibitisha kuwa serikali inaunga mkono ombi la Kenya la kuwa mwenyeji wa raundi ya HSBC ya daraja la pili mwezi Februari 2026. “Tuko tayari kwa changamoto hiyo,” alisema. “Serikali itahakikisha msaada kamili wa kiufundi na kiusalama ili mashindano yafanyike kwa mafanikio.”

Mwenyekiti wa KRU, Harriet Okach, aliwahimiza mashabiki kujaza uwanja wa RFUEA mnamo Novemba 15–16 kushangilia Lionesses.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KRU, Thomas Odundo, aliongeza kuwa ombi la Kenya la kuwa mwenyeji wa mashindano ya HSBC Division II tayari limepata baraka za wizara.

Wadhamini wakuu pia walithibitisha kuendelea kwao kusaidia timu. Francis Gitonga wa Coca-Cola Beverages Africa alisema, “Tunajivunia kuunga mkono raga ya wanawake kama wadhamini wa vinywaji.”

Timu ya Kenya Lionesses. Picha|Geoffrey Anene.

Andrew Mathu wa Safaricom M-Pesa aliongeza, “Tunafurahia kudhamini Lionesses. Kipaumbele chetu ni ustawi wao na maendeleo ya mchezo.”

Nahodha wa Lionesses, Sheila Chajira, pamoja na manahodha wa zamani Janet Okello na Grace Okulu, waliwahimiza Wakenya kujitokeza kwa wingi. “Mwambie rafiki amwambie rafiki aje atutazame tukicheza,” alisema Chajira.

Lionesses wanawinda taji lao la pili la Afrika tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2006. Kenya ilinyakua ubingwa wa mwaka 2018 kwa kuilaza Uganda 29–7, lakini imepoteza mara 13 kwenye fainali, ikiwemo mara saba mfululizo dhidi ya Afrika Kusini.

Lionesses walizidiwa nguvu 12–7 na 17–10 katika fainali mbili zilizopita dhidi ya Afrika Kusini.

Nchi 12 zitashiriki katika mashindano ya mwaka huu ambapo Kenya inalenga kurejesha taji na kuthibitisha nafasi yake kama taifa kinara cha raga ya wanawake barani Afrika.