Habari

Mkurugenzi wa Uhariri wa NMG sasa ni Dkt, apata PhD

Na STANLEY NGOTHO November 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MKURUGENZI wa Uhariri wa Nation Media Group (NMG), Joe Ageyo, alikuwa miongoni mwa mahafala 29 waliotunukiwa jana shahada ya uzamifu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Daystar mjini Athi River, Kaunti ya Machakos.

Safari ya Dkt Ageyo kutunukiwa shahada hiyo katika masuala ya uanahabari ilisimamiwa na Prof Levi Obonyo na Dkt Lydia Radoli. Kilele cha usomi wake huo kilikuwa uwasilishaji wa tasnifu iliyojikita katika uchanganuzi wa mijadala kuhusu mabadiliko ya tabianchi katika magazeti ya humu nchini kutokana na mikutano minne tofauti ya COP.

Katika hali yake ya kawaida ya utulivu, Dkt Ageyo, ambaye ni mwanahabari nguli anayejivunia mafanikio tele kitaaluma kwa zaidi ya miongo miwili, alisubiri kwa saa nyingi kabla ya wakati wake wa kutunukiwa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Daystar, Dkt Florence Muindi, kufika.

Alipoitwa, alipanda jukwaani kwa furaha akijivunia ufanisi uliokuwa zao la kujinyima ikizingatiwa wingi wa majukumu yake katika chumba cha habari na uzito wa kazi za darasani alizozishughulikia kwa miaka kadhaa.

“Kiu ya kutaka kuimarisha ujuzi wangu katika tasnia ya habari ilinichochea kurejea darasani. Taaluma ya uanahabari imepitia mabadiliko makubwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita,” alitanguliza Dkt Ageyo.

“Mazingira ya usambazaji wa habari yamebadilika sana duniani kote. Sekta hiyo inahitaji fikira mpya ndipo wadau wafaulu kunasa hadhira lengwa kwa taarifa za kuthibitishika zilizofanyiwa utafiti wa kina,” akaongeza.

“Nawahimiza wanahabari wenzangu – vijana kwa wazee – kutenga muda ili wajikuze zaidi katika safari ya elimu. Kadri watakavyosoma ndivyo watavyogundua kwamba kuna mengi ambayo wamekuwa wakiyakosa sana katika vyumba vya mihadhara vyuoni,” akasisitiza Dkt Ageyo.

Ni katika mahafali ya jana chuoni Daystar, ambapo pia Meneja wa Udhibiti wa Ubora wa NTV Alfred Chomba na Meneja wa Mitandao ya Kijamii katika NMG Mitchell Namasaka walitunukiwa shahada ya uzamili katika uanahabari na shahada ya kwanza katika uhusiano wa umma na mawasiliano mtawalia.