Jamvi La Siasa

Mbunge amkabili Ruto peupe kwa kuita upinzani watu bure kabisa

Na BENSON MATHEKA November 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Mbunge wa Makueni, Suzanne Ndunge Kiamba alionyesha ujasiri wa kipekee kwa kumkabili Rais William Ruto ana kwa ana kuhusu tabia yake ya kuendelea kuita viongozi wa muungano wa upinzani watu bure kabisa wasio na ajenda yoyote kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara ya maendeleo ya Rais Ruto eneo la Ukambani Jumatano, Novemba 12, 2025, mbunge huyo alionekana kuchoshwa na kauli za rais kudai kuwa viongozi wa upinzani hawana maana.
Mbunge huyo alimwambia rais kwamba anapaswa kuwaheshimu viongozi wa upinzani na kuacha mtindo wa kuwadharau kwa kusema ni watu bure kabisa.
Kulingana na mbunge huyo, kila binadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu, na kutumia lugha kama hiyo ni kinyume cha mafundisho ya Kikristo. Alimtaka Rais kuwaheshimu wanasiasa wengine hata kama hawamuungi kisiasa.
“Hakuna mtu aliyeumbwa kwa sura ya Mungu anaweza kuwa bure kabisa; kila mtu ameumbwa kwa sura ya Mungu. Hata awe bubu, ana kitu ndani yake. Hii ya kutuambia sisi tukiwa upinzani eti sisi ni bure kabisa siipendi. Wakati tunafanya siasa, tupeni nafasi; tuwe na heshima,” Bi Kiamba alimwambia Rais.
Rais hakusita kumjibu. Alidai kuwa si yeye anayewaita viongozi wa upinzani bure kabisa bali ni Wakenya wenyewe ambao, kwa mujibu wa Ruto, baada ya kugundua kuwa upinzani hauna ajenda ya maana, wameanza kuwaita bure kabisa.
Katika ziara hiyo, viongozi wanaomuunga Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka waliandamana na Rais kuzindua miradi kadhaa ya serikali katika kaunti hiyo lakini ni mbunge huyo aliyekuwa na ujasiri wa kumkosoa wazi wazi.
Kiongozi wa nchi alifanya ziara ya siku nne eneo la Ukambani, ngome ya kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka mmoja wa vinara wa upinzani.
Japo Bw Musyoka na vinara wengine wa upinzani wamekuwa wakimkosoa Rais hawajahi kufanya hivyo mbele yake alivyofanya mbunge huyo.