Pambo

Tabia ndogo zinazoyeyusha mahaba katika ndoa

Na BENSON MATHEKA November 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Kukolezana mapenzi hujenga ndoa yenye furaha. Hata hivyo, tabia fulani za kila siku zinaweza kuua mahaba bila mume na mke  kujua.

Wataalamu wa mahusiano wanasema kwamba uhusiano wa kimapenzi haujengwi tu kwa zawadi wala maneno matamu, bali kwa kuelewana na kuheshimiana kila siku.

Hivyo, ni muhimu kutambua tabia zinazoyeyusha hisia za mahaba kati ya wanandoa na kujifunza kuziepuka.

Wataalamu wa masuala ya mahusiano wanasema kuendelea kuchelewa kurudi nyumbani kiholelea au kutoonyesha uwepo wa kihisia kunapunguza upendo kati ya wanandoa.

Mke au mume anapohisi kupuuzwa, hisia za upendo hupungua. “Muda wa kuwa pamoja ni mtaji wa mahusiano; ukikosa, uhusiano huanza kuyumba, asema mtaalamu wa masuala ya ndoa, Dkt Laura Berman.

Anasema ukizoea kumpa mpenzi wako zawadi za kifahari na ukose muda wa kuwa naye, unafanya kazi bure.

“Zawadi haziwezi kuunda mvuto wa kweli. Mke au mume anapopata hisia kuwa mpenzi anamjali kihisia, hakuna zawadi inayoweza kumpendeza zaidi. Tabia za dhati za kuonyesha upendo kwa hisia ni msingi wa mvuto wa kimapenzi, sio zawadi,” asema.

Kulingana na mwanasaikolojia Esther Perel, shaka au hofu kuhusu uaminifu huharibu mahusiano.

 “Uaminifu ni msingi wa mvuto wa kimapenzi ndani ya ndoa. Hivyo, waume na wake wanashauriwa kushirikiana kwa uwazi na kudumisha uaminifu kila wakati,” asema Perel. Anasema watu huua mahaba katika ndoa kwa kuyadai kwa nguvu kwa kuwa ni haki yao.

“Kudai mapenzi kama haki badala ya kuunda hali ya upendo huweza kuumiza mpenzi. Mahusiano ya kweli hufanikishwa kupitia mwaliko wa kimapenzi na kusherehekea na kuburudika pamoja. Wanaume wanapaswa kuelewa kuwa mapenzi hayadaiwi kwa nguvu, bali  hukaribishwa na kupaliliwa,” aeleza Perel.

Mtaalamu wa masuala ya mahusiano Dkt John Gottman anasema tabia ya wanandoa kupuuza ishara za upweke  inaweza kuyeyusha mapenzi kabisa.
“Wakati mwingine, mpenzi wako anakosa hamu ya kufanya mapenzi kwa sababu amechoka au ana tatizo. Tabia ya kumlaumu au kumshinikiza inaweza kuua mvuto,” asema  Gottman.

“Heshimu hisia za mpenzi wako; jinsi unavyomtendea leo ndilo litakaloamua mapenzi yake kesho kwako,” asema.
Unavyomtendea mpenzi wako kunaamua kiwango cha hisia za mapenzi kwako.

“Tabia za mke zinahusiana sana na anavyotendewa na mumewe. Kumpinga, kumkashifu, au kuwa na huzuni mara nyingi huondoa hamu. Badala yake, tabia za urafiki, uratibu wa kimapenzi, na kuonyesha upendo kwa vitendo ndizo zinazoongeza mvuto wa kimapenzi,” asema Perel.

Kulingana na Laura, tatizo lolote linalokuzuia kutamani mapenzi lazima lijadiliwe haraka. Usihofie kuzungumza kuhusu mapenzi, hisia, au changamoto na mume au mke wako.

“Kuwasiliana kwa uwazi kunaunda kinga dhidi ya kutoelewana na kuchemka kwa hisia,” aeleza Laura.

Kulingana na mtalaamu huyu, tabia ndogo zinazopuuzwa zinaweza kuua mahaba, lakini zinazoshughulikiwa kwa hekima huimarisha upendo.

Kujali hisia za mpenzi, kudumisha uaminifu, na kuwasiliana kwa uwazi ni msingi wa mahusiano yenye afya na furaha kwa muda mrefu.