Habari

Nani anayeua wazee Salgaa?

Na MERCY KOSKEI November 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

POLISI katika eneo la Salgaa, Kaunti ya Nakuru wameanza uchunguzi na kuwaandama waliotekeleza mauaji ya wazee watatu ndani ya muda wa wiki mbili.

Mauaji hayo ya kushangaza yamewashangaza wenyeji ambao wanawataka polisi kuwanyaka waliohusika ili kuzuia visa kama hivyo siku zijazo.

Wiki moja tu baada wanandoa wawili wakongwe kuuawa nyumbani kwao kijijini Muthera, polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu mauaji ya ajuza mmoja ambaye mwili wake ulipatikana ndani ya nyumba yake wikendi.

Marehemu Margaret Wambui, 65 ambaye ni mwanachama wa kundi la wanawake wa Kanisa la PCEA, alipatikana nyumbani kwake akiwa na majeraha mabaya ya kichwa mnamo Ijumaa wiki jana.

Kwa mujibu wa mwanawe Rahab Wanjiru, siku hiyo alijaribu kumpigia mamake simu lakini ikawa imezimwa.

Bi Wanjiru, mkazi wa eneo la Bluegem, Salgaa, aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa alikuwa akisubiri mamake ampigie simu ndipo akapokea simu kutoka kwa shangaziye kwamba mamake alikuwa ameuawa.

“Shangazi yangu akiwa na afisa wa Nyumba Kumi, aliniambia kuwa nilihitaji kufika katika Kituo cha Polisi cha Salgaa lakini hata kabla hatujaondoka alituambia habari hizo za mauti. Aliniambia mamangu aliuawa na lazima nifike kabla ya mwili wake kupelekwa chumba cha kuhifadhi maiti,” akasema.

“Hatujaambiwa chochote na makachero ambao walikuja nyumbani kwetu wikendi iliyopita. Bado tunasubiri japo kipande cha mbao ambacho kinaaminika alipigwa nacho kilichukuliwa siku ambayo mwili wake ulipelekwa mochari,” akaongeza.

Kwa mujibu wa Bi Wanjiru, uchunguzi wa maiti unaonyesha kuwa mamake aliaga dunia kutokana na majeraha ya kichwa na pia fuvu lake liliharibiwa, mkono wake ukavunjwa mara tatu ishara kuwa alikuwa akipambana na wauaji wake.

Wiki mbili zilizopita miili ya Joseph Ndegwa Kihiti, 90 mchungaji wa kanisa na mkewe Rose Wanjiku, 63 ilipatikana ndani ya nyumba yao Rigogo, Novemba 2.

Wawili hao walikosa kufika kanisani na kusababisha wanakijiji waanze kuwasaka.

Uchunguzi wa upasuaji wa maiti kwenye miili yao uliofanywa siku sita zilizopita, umeonyesha kuwa wawili hao waliaga dunia kutokana na majeraha ya kupigwa kwa kifaa butu. Mikono ya Bw Kihiti na bega lilikuwa limevunjika ishara kuwa naye pia alikuwa akipambana na wauaji wake.

Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi (DCI) Donnata Otieno alithibitisha matukio hayo mawili.