Habari

Polisi wamwagwa Mbeere North kampeni za ubunge zikichacha

Na GEORGE MUNENE November 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

POLISI waliojihami vikali wamemwagwa Mbeere Kaskazini huku taharuki ikiendelea kutanda wakati ambapo kampeni za uchaguzi mdogo zimeingia mkondo wa lala salama.

Maafisa wa usalama sasa wanaonekana wakipiga doria kwenye masoko na maeneo mbambali katika eneobunge hilo ambalo ni kame.

Mirengo ya serikali na upinzani imekuwa ikishutumiana kwa kupanga ghasia wakati huu ambapo kampeni zimechacha kuelekea uchaguzi wa Novemba 27.

Viongozi wa upinzani wakiongozwa na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua nao wanadai kuwa UDA imekuwa ikiwatumia wahuni kuvuruga mikutano yao ya kisiasa.

“Tunafahamu yanayoendelea na hatutatikisika,” akasema Bw Gachagua.

Kila mrengo unang’ang’ania maeneo ya kufanya kampeni. UDA imekuwa ikiendesha kampeni maeneo ambayo upinzani ushafanya hadhara zake, hali ambayo imewakasirisha viongozi wa upinzani.

“Wanasiasa wa UDA wanatufuata maeneo ambako tumefanya kampeni. Wanatuchokoza ila tutasalia watulivu na hatutashiriki ghasia,” akasema Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji.

Mnamo Novemba 16, 2025, maafisa wa UDA pamoja na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku waliandaa mikutano maeneo yote ambako upinzani ulikuwa umetembelea.

Katika kituo cha Kibiashara cha Kanyuambora, wafuasi wa upinzani na wale wa serikali nusura wakabiliane lakini maafisa wa usalama wakaingilia kati.