Habari

Walimu wakuu wapinga kuongozwa na walimu wa JSS

Na WINNIE ATIENO November 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

CHAMA cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi (KEPSHA) na Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) vimepinga uongozi mpya unaopendekezwa ambapo walimu wa Shule za Sekondari ya Chini (JSS) msingi ‘kusimamia’ walimu wakuu wa shule za msingi.

Viongozi wa vyama hivyo, viwili wameilaumu Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kwa kupanga kutekeleza mabadiliko hayo ilhali wengi wa walimu wa JSS ni wale waliohitimu juzi na hawana tajriba katika taaluma ya ualimu.

Wamesema mpango huo mpya haufai kutekelezwa kwa sababu utazua mvutano wa kila mara.

Haya yanajiri wakati ambapo Mkurugenzi wa TSC anayesimamia uajiri, Bi Antonina Lentoijoni amethibitisha mipango ya tume hiyo kuanzisha mfumo mpya wa usimamizi katika shule za msingi na shule za sekondari msingi zilizoko pamoja.

Kwa mfano, shule hizo zitakuwa na manaibu wawili wa mwalimu mkuu ambapo mmoja atasimamia shule ya msingi na mwengine anayeongoza shule ya sekondari msingi (JSS).

Kuna jumla ya walimu 89,000 walioajiriwa kufundisha katika jumla ya shule 20,000 za JSS.

Lakini lwa muda wa miaka mitatu, walimu wakuu na walimu wa JSS wamekuwa wakizozana.

“Hadi pale tutakapoweka muundo wa uongozi unaokubalika kisheria, walimu wakuu watatusaidia kwa sababu wanao mwongozo wa kushughulikia hali hiyo. Wakati huu, wangali wanatusaidia kusimamia shule za JSS,” akasema Bi Lentoijoni.

Lakini Mwenyekiti wa Kepsha Faud Ali alipuuzilia mbali pendekezo hilo, akisisitiza kuwa walimu wa JSS sharti waheshimu muundo wa uongozi ulioko sasa.

“Hatutaki siasa katika shule zetu. Aidha, uheshimu uongozi wa sasa katika shule jumuishi au uende ukafundishe katika shule za sekondari pevu,” akasema Bw Ali, ambaye pia ni Mwalimu Mkuu wa Nairobi Comprehensive School (zamani Nairobi Primary).

Aliongeza kuwa walimu wa JSS wanafaa kuhudumu katika Shule za Sekondari Pevu.

“Unaweza kuhama na wanafunzi wa Gredi 9 hadi katika Shule ya Sekondari Pevu. Hiyo ndio njia ya kipekee utuheshimu au uhamie shule za sekondari pevu,” akaeleza.