Afueni wakazi wa ardhi inayozozaniwa Kibiko wakipata barua za umiliki
Ni afueni kwa wakazi wa Kibiko, Ngong katika eneobunge la Kajiado West baada ya kupokea barua za umiliki wa ardhi ya mababu zao kufuatia zaidi ya miaka ishirini ya migogoro ya uongozi, mkanganyiko, wasiwasi na ukosefu wa usalama.
Ardhi hiyo ya jamii yenye ukubwa wa ekari 2,800 imekuwa kitovu cha mvutano wa uongozi kati ya makundi mawili, jambo lililochelewesha kugawa ardhi hiyo kwa wanachama wake. Kundi moja linaongozwa na Mwenyekiti wa muda mrefu, Moses Parantai, huku lingine likiongozwa na Moses Monik, kila moja likidai kuwa na uungwaji mkono mkubwa wa wanachama.
Hivi majuzi, eneo hilo limekumbwa na ongezeko la visa vya ukosefu wa usalama vinavyohusisha wamiliki wa ardhi na madai ya kuwepo kwa magenge yanayoshirikiana na baadhi ya viongozi wa eneo hilo katika njama ya kuinyakua ardhi.
Wakazi wa ranchi hiyo yenye thamani ya Sh100 bilioni, ambao wameishi katika ardhi hiyo kwa miaka mingi, wamekuwa wakihofia kufurushwa kutokana na vitisho kutoka kwa watu wanaojulikana na wasiojulikana.
Hata hivyo, mchakato wa kupanga upya wanachama umechukua mkondo mpya mwezi mmoja baada ya kundi la Bw Monik kutoa hati miliki 4,500, na wanachama waliokosa kuridhika wakipokea barua za umiliki kutoka kwa Bw Parantai siku ya Jumatatu, hatua iliyozidisha mpasuko.
Bw Parantai alitaja barua hizo za umiliki kama zinazorejesha matumaini kwa wanachama wanaosubiri hati miliki halisi kutoka kwa Wizara ya Ardhi mapema mwaka ujao.
“Washindani wetu wamekuwa wakitoa hati miliki za kughushi kwa wanachama walioteuliwa kwa upendeleo. Sisi tunatoa barua za umiliki kutoka serikali ya kaunti kwa wanachama halisi. Kila mwanachama atapata ekari moja. Hakuna mtu atakayehamishwa kutoka anakoishi,” alisema Bw Parantai.
Wanachama wamepongeza zoezi hilo kama la uwazi, wakisema walionufaika ni wanachama wanaofahamika wa ardhi ya jamii, na wakasisitiza kuwa zoezi lilifanywa kwa usawa.
Wajane, mayatima na wazee walikuwa miongoni mwa wanachama waliosherehekea hatua hiyo.
“Tumepata tena matumaini ya kuishi katika ardhi hii baada ya miaka ya hofu ya kufurushwa. Mchakato huu ni wa wazi na unaozingatia utu,” alisema Flora Nkalu, mwanachama.
Katika awamu ya kwanza, barua 4,600 za umiliki zilitolewa, na walionufaika wanatarajia kuwa mchakato wa kupata hati miliki utaharakishwa.