Wachezaji wawili wa Harambee Starlets kukosa mechi ya kupimana nguvu dhidi ya Algeria
WACHEZAJI wawili muhimu wa timu ya taifa ya soka ya mabinti Harambee Starlets, watakosa mechi mbili za kupimana nguvu dhidi ya Algeria Novemba 26 na 30 mjini Bilda, Algeria.
Beki Tabitha Amoit na kiungo Lavender Akinyi ambao wanatumikia timu ya Ulinzi Starlets ya Ligi Kuu ya Warembo ya Shirikisho la Soka Nchini (FKF-WPL) hawatakuwepo kwani, wameanza mafunzo ya miezi sita kujiunga jeshi katika Shule ya Mafunzo ya Uajiri ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (DFRTS) mjini Eldoret.
Wawili hao walikuwa muhimu katika kuisaidia Starlets kufuzu kwa michuano ya Kinadada ya Mataifa ya Afrika (WAFCON) 2026 mwezi jana, baada ya miaka 10. Starlets walivuna ushindi wa 4-1 wa jumla ya mabao dhidi ya Gambia katika raundi ya pili na ya mwisho ya kufuzu dimba hilo.
Jana (Jumanne), kocha Beldine Odemba alitaja kikosi cha wachezaji 23 ambao watawakilisha taifa katika mechi hizo.
Katika kikosi hicho, Odemba amefanya mabadiliko kadhaa. Viungo Emily Moranga na Providence Mukalo, washambuliaji Valerie Nekesa na Euphraiser Shilwatso wanarejea kikosini.
Beki Sheryl Muyera anaye chezea Zetech Sparks ya FKF-WPL, amejiunga na Starlets kwa mara ya kwanza.
Odemba ambaye alitajwa kama kocha bora wa mwezi Oktoba na Chama cha Wanahabari wa Michezo nchini (SJAK), atatumia mechi hiyo kama maandalizi ya michuano ya WAFCON ambayo itaandaliwa nchini Morocco Marchi 17 hadi Aprili 3.
Algeria iliyo nafasi ya 80 katika viwango vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) pia ilifuzu WAFCON baada ya ushindi wa 3-1 wa jumla ya mabao dhidi ya Cameroon.
Sasa watacheza katika michuano hiyo kwa mara ya nane ikilinganishwa na Kenya (nafasi ya 140 viwango vya FIFA) ambao watashiriki kwa mara ya pili.
Kikosi cha Starlets kinatarajiwa kuingia kambini Ijumaa hii na kuondoka kuelekea Algeria Jumapili.
Walinda lango
Annedy Kundu, Lilian Awuor
Mabeki
Lorine Ilavonga, Leah Andiema, Sheryl Muyera, Ruth Ingosi, Vivian Nasaka, Dorcas Shikobe, Enez Mango
Viungo wa kati
Medina Abubakar, Providence Mukalo, Corazone Aquino, Martha Amnyolet, Elizabeth Muteshi, Fasilah Adhiambo
Washambuliaji
Euphraiser Shilwatso, Valerie Nekesa, Mwanalima Adam, Catherine Khaemba, Elizabeth Wambui, Shirleen Opisa, Airin Madalina, Emily Morang’a