Jamvi La Siasa

Uhuru anavyopangua hesabu za Ruto, Gachagua 2027 kwa kumnadi Matiang’i Mlima Kenya

Na CHARLES WASONGA November 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UREJEO wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta katika ulingo wa siasa unaonekana kuzua tumbojoto katika kambi ya Rais William Ruto.

Kando na hayo, hatua hiyo pia inaonekana kuvuruga mikakati ya kisiasa katika Umoja wa Upinzani, haswa ya vinara wake, Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Juzi, Bw Kenyatta aliongoza mkutano mkubwa wa hadhara wa chama chake cha Jubilee katika kaunti ya Murang’a akiandamana na mgombea urais wa chama hicho Fred Matiang’i , jukwaa alilolitumia kurusha cheche za mashambulio kwa serikali ya sasa ya Dkt Ruto.

Huku akionekana kumpigia debe Dkt Matiang’,  rais huyo mstaafu aliwataka wakazi wa Mlima Kenya kutokaidi ushauri wake walivyofanya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 kwa kuupigia kumpigia kura rais wa sasa.

“Niliwaonya wakati ule lakini hamkusikia na kuamkia kuchagua hawa watu. Si sasa mwajionea?” Bw Kenyatta akasema, bila kutoa ufafanuzi zaidi.

Ufasiri wa kauli yake ni kwamba endapo wakazi wangeunga mkono chaguo lake wakati huo, Raila Odinga, hawangekuwa wakilalamika wanavyofanya sasa.

Bw Kenyatta aliwaraia wakazi kumunga mkono Dkt Matiang’i akimtaja kama kiongozi mwenye maono na mchapa kazi anayeweza kukamilisha miradi ya maendeleo ambayo yeye mwenyewe alianzisha wakati wa utawala wake na ambayo hayajakamilishwa.

“Mnamo 2022 niliwaonya kuhusu watu fulani lakini hamkusikia. Sasa nitumai kuwa mko tayari kuwaunga viongozi ambao wamejitolea kwa dhati kuleta kusukuma gurudumu la maendeleo nchini Kenya,” akaeleza.

Kauli hiyo ya Bw Kenyatta sasa imewakera wandani wa Rais Ruto wanaoifasiri kama inayohoji uwezo na sera za maendeleo za  serikali ya Kenya Kwanza wakati ambapo inajizatiti kujinadi kwa raia iweze kupewa nafasi kuendelea baada ya 2027.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei  na Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi wamejitokeza na kumwonya Bw Kenyatta dhidi ya kuendelea kuchapa siasa ilhali “serikali yake ilifeli kutekeleza maendeleo yenye manufaa kwa umma kama yale ya Rais wetu.”

Aidha, Bw Cherargei ameonya kwamba endapo Bw Kenyatta hatakoma kuikosoa serikali ya Rais Ruto, malipo yake na manufaa mengineyo yatakatizwa.

“Tafadhali Bw Kenyatta kaa nyumbani na utazame jinsi serikali ya Rais Ruto inavyotekeleza sera za kufaidi raia katika sekta za afya, elimu, barabara na mengineyo. Ukiendelea kuingilia serikali utapokonywa walinzi pamoja na malipo unayopokea sasa baada ya kustaafu. Hauwezi kuendelea kufurahia rasilimali za serikali ilhali inaipiga vita,” akaonya.

Hata hivyo, Profesa Gitile Naituli anashikilia kuwa serikali haiwezi kukatiza malipo ya Bw Kenyatta na kumpokonya walinzi “kwa sababu hii ni haki yake ya kikatiba kupewa mafaayo hayo”.

“Nani alimwambia Seneta Cherargei kwamba serikali inaweza kumzuia Bw Kenyatta kufurahia haki zake za kisiasa kwa mujibu wa Kipengele cha 37 cha Katiba kwa misingi kwamba yeye ni Rais mstaafu. Akumbuke kuwa Bw Kenyattaa angali kiongozi wa chama cha Jubilee ambacho kimemteua Dkt Matiang’I kama mgombeaji wake wa urais. Kwa hivyo, yuko huru kumnadi mwanasiasa huyo haswa katika ng’ome yake ya Mlima Kenya,” anaeleza msomi huyo, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

Hata hivyo, Profesa Naituli anaungama kuwa kwa kumpigia debe Dkt Matiang’i katika eneo la Mlima Kenya, Bw Kenyatta amekwaza kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizen Party (DCP) Rigathi Gachagua.

“Bila shaka kambi ya Gachagua imefasiri hatua hiyo ya Bw Kenyatta kama uchokozi ikizingatiwa kuwa naibu huyo wa rais wa zamani ameshikilia kuwa ndiye atatoa mwelekeo wa siasa kwa wakazi wa Mlima Kenya kuelekea 2027,” akasema.