Habari

Ziko wapi? Hofu Sh12.6B za Hasla Fund zimekunywa maji

Na DAVID MWERE November 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WABUNGE wameibua wasiwasi kuhusu kulipwa kwa Sh12.6 bilioni zilizokopeshwa wananchi kupitia Hazina ya Hustler Fund.

Wabunge hao sasa wanataka ukaguzi maalum ufanywe kutokana na madai ya ukosefu wa mifumo madhubuti ya ulinzi wa fedha hizo.

Hofu ya kupotea kwa mabilioni hayo ilijitokeza wakati Waziri wa Ushirika Bw Wycliffe Oparanya, pamoja na Katibu wa Wizara hiyo Susan Mangeni walipofika mbele ya Kamati ya Hazina Maalum ya Bunge la Kitaifa kujibu maswali hukusu usimamizi wapesa hizo.

Haya yalijiri baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Hustler Fund, Bw Henry Tanui, kuwajulisha wabunge kuwa kati ya Sh14 bilioni za hazina hiyo, ni Sh1.4 bilioni pekee zinatolewa kama mkopo.

“Kufika hapa bila kujibu swali lolote ni dhihaka kwa kamati hii. Ukisema hakuna pesa zimepotea, basi huishi Kenya,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Migori, Bi Fatuma Mohammed.

Kulingana na Ofisi ya Bajeti ya Bunge (PBO), Sh12.6 bilioni zinaweza kujenga angalau kilomita 12 za Barabara ya Rironi–Mau Summit, au kugharamia masomo ya wanafunzi 566,000 wa sekondari kwa kiwango cha mgao  sasa cha Sh22,240 kwa mwanafunzi.

Maswali makuu ya wabunge yalihusu kiasi halisi kilichokopeshwa, ni kiasi gani kimerejeshwa, na iwapo fedha zozote zimepotea.

Hata hivyo, kikao kilichukua mkondo tofauti baada ya Bw Tanui kukosa kuwasilisha stakabadhi za walionufaika licha ya agizo la kamati.

Kutokana na hilo, Mbunge wa Imenti Kaskazini, Rahim Dawood, alitaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum.

Alilalamika kuwa maombi ya kamati kupata orodha ya wanaonufaika yamepuuzwa.

“Vyombo vya habari vinaripoti kuwa wengi waliochukua mikopo hawajulikani wala hawawezi kufuatiliwa. Hizi pesa zimepotea,” akasema Bw Dawood.

Mbunge wa Mwingi Magharibi, Charles Nguna, naye alikiri kuwajua watu waliochukua mikopo kwa kutumia laini mpya kisha kuzifunga bila nia ya kulipa.

Hata hivyo, Bw Tanui alisisitiza kuwa hakuna pesa zilizopotea na akaahidi kuwasilisha majina ya wakopaji ndani ya siku saba.

Wabunge walisema kuwa suala hilo linagusa moja kwa moja Hazina ya mlipa ushuru, na hivyo linafaa kutatuliwa kwa uwazi bila kuficha taarifa zozote.

Waliongeza kuwa Hustler Fund ilizinduliwa kama msaada wa kuwainua vijana na wafanyabiashara wadogo, hivyo kutopatikana kwa taarifa za wakopaji kunadhoofisha imani ya umma kwa mpango huo.

Bi Mohammed aliitaka Wizara ya Ushirika kueleza sababu za kupungua kwa kiwango cha fedha zinazotolewa kama mkopo kutoka Sh14 bilioni hadi Sh1.4 bilioni pekee, akisema tofauti hiyo ni kubwa mno na haiwezi kufichwa kwa majibu mafupi.

“Kama kweli hakuna pesa zimepotea, basi tupate thibitisho kwa maandishi. Kinyume na hapo, tutaamini kwamba kuna udhaifu mkubwa katika usimamizi wa fedha hizi,” alisema.

Wabunge wengine walishangaa kwa nini mfumo wa udhibiti haukuimarishwa kabla ya kuanzishwa kwa mpango huo, ilhali serikali ina mifumo ya kielektroniki na usajili wa simu kwa kutumia kitambulisho cha kitaifa.

Walidai kwamba kama serikali ina uwezo wa kufuatilia laini haramu za simu, basi haipaswi kushindwa kufuatilia walionufaika wa mikopo.