Makala

UN yataka uchunguzi ufanywe kuhusu mauaji nchini Tanzania

Na WINNIE ONYANDO Na MASHIRIKA November 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UMOJA wa Mataifa (UN) umetoa wito uchunguzi ufanywe kuhusu vifo vya mamia ya watu waliokuwa wakiandamana kupinga uhalali wa uchaguzi nchini Tanzania.

Kamishna Mkuu wa UN anayesimamia Haki za Binadamu, Volker Türk, alisema kumekuwa na jaribio la kuficha ushahidi na ukweli kufuatia ripoti kwamba polisi walikuwa wakichukua miili kutoka vyumba vya kuhifadhia maiti na kuipeleka maeneo yasiyojuilikana.

Turk aliitaka serikali ya Tanzania kuachilia miili hiyo na kuikabidhi kwa familia zao ili ipumzishwe.

Haya yanajiri huku chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, kikidai kuwa watu wapatao 1,000 waliuawa kwenye maandamano hayo yaliyozuka siku ya uchaguzi mnamo Oktoba 29.

Hadi sasa, serikali haijatoa idadi kamili ya vifo vilivyotokea katika maandamano hayo.

UN inasema kuwa mamia ya watu wanaaminika kuuawa lakini imesema haijaweza kuthibitisha idadi rasmi kutokana na hali ilivyo tete nchini Tanzania, ambako huduma za intaneti zilikatwa kwa siku sita baada ya uchaguzi.

Msemaji wa serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, hakujibu ombi la Reuters la kumtaka atoe maoni yake.

Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imesema idadi ya vifo vya upinzani imetiwa chumvi lakini haijaweka wazi idadi yake ya waliofariki.

Samia alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa mwezi uliopita, baada ya kupata karibu asilimia 98 ya kura.

Wapinzani wake wawili wakuu walikuwa wameondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho.

UN hapo awali ilisema mnamo Oktoba 31 kwamba ilikuwa na ripoti kwamba watu wasiopungua 10 waliuawa katika miji mitatu.

Hata hivyo, ilisema: “Taarifa zilizopatikana na Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kutoka vyanzo tofauti nchini Tanzania zinaonyesha kuwa mamia ya waandamanaji na watu wengine waliuawa na idadi isiyojulikana kujeruhiwa au kuzuiliwa.”

Hapo awali, serikali ilikanusha kuwa maafisa wa usalama walitumia nguvu kupita kiasi na imesema walikuwa wakidhibiti ghasia za wahalifu.

Mnamo Novemba 10, 2025, polisi waliwaachilia kwa dhamana viongozi wanne wakuu wa upinzani akiwemo makamu mwenyekiti wa CHADEMA.

Zaidi ya watu wengine 300 wameshtakiwa kuhusiana na maandamano hayo, wakiwemo takriban 145 kwa kosa la uhaini.Kiongozi wa CHADEMA, Tundu Lissu, alishtakiwa kwa uhaini mwezi Aprili mwaka huu.

Kuzuiwa kwake kuwania kiti cha urais ni miongoni mwa matukio makuu yanayoaminika kuchochea maandamano.Wapinzani wa Samia wameishutumu serikali yake kwa kukandamiza upinzani na kuwateka nyara wale wanaoikosoa serikali yenyewe.

Waangalizi kutoka Umoja wa Afrika wiki iliyopita walisema kuwa uchaguzi huo haukuonyesha demokrasia na ulikosa haki na usawa.