Mchakato wa kutunga sheria hautakuwa wa gharama ya juu sasa
MCHAKATO wa kutunga sheria katika Bunge la Kitaifa na lile la Seneti sasa hautakuwa ya gharama ya juu ikiwa mswada wa Sheria ya Ushirikishaji wa Umma wa 2025 (marekebisho) utapitishwa.
Kulingana na mswada huo, sasa haitakuwa lazima mchakato wa kushirikisha umma ufanywe mara mbili.
Mabunge ya Kitaifa na Seneti, yatakuwa na uamuzi wa kuzuia kurudiwa kwa mchakato wa kushirikisha umma kwenye sera ya umma au suala la kutunga sheria linalohusu mabunge hayo mawili ikiwa sheria inayopendekezwa itapitishwa.
Mswada wa Sheria ya Ushiriki wa Umma wa 2025, unaozingatia utumizi wa busara na uwajibikaji wa rasilimali za umma, unafuata pendekezo la Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, kwamba ushirikishwaji wa umma na mabunge hayo mawili kuhusu mswada unahitaji maridhiano.
Spika alibainisha kuwa ushirikishwaji wa umma unaweza kushughulikiwa na kamati ya bunge inayoanzisha mswada au hati ya sera ya umma na nyingine ikishiriki.
Mswada huo unaodhaminiwa na Wabunge Dkt Otiende Amollo (Rarieda) na Samuel Chepkonga (Ainabkoi) ulioko kwenye Bunge la Kitaifa kwa sasa, unalenga kufafanua upeo na mbinu za ushiriki wa umma kuhusu miswada na stakabadhi nyingine za sera za umma zinazoletwa bungeni ili kuchakatwa.
Mswada huo pia unapendekeza kuimarisha, kukuza na kuwezesha ushiriki wa wananchi katika utawala huku ukizitaka mamlaka zinazohusika kuandaa taratibu mahususi ndani ya muda uliowekwa ili kuongoza mchakato huo.
Kifungu cha pili cha mswada kinafafanua “ushiriki wa umma” kama mchakato wa kuhusisha umma katika kufanya au kutekeleza maamuzi ya sera ya umma ikiwa ni pamoja na kutunga sheria.
Pia inapendekeza mamlaka zinazowajibika na kuzipa mamlaka ya kushiriki kwa umma pamoja na kuandaa miongozo mahususi ya ushiriki wa umma.
“Rasilimali za umma zitatumika kwa njia ya busara na uwajibikaji. Kamati ya Bunge inaweza kuchukua hatua ili kuepuka kurudia mchakato huo unaofanywa na kamati ya bunge tangulizi,” mswada huo ulisema.
Hivi sasa, kamati husika hushirikisha umma na ikiwa itapitishwa, basi kamati ya bunge pia inafanya mchakato nyingine ya kushirikisha umma.