Pesa Otas: Mamilioni yanywa maji chaguzi ndogo
UAMUZI wa Rais William Ruto kuwateua wabunge sita waliokuwa wakihudumu kujiunga na Baraza lake la Mawaziri umeigharimu nchi zaidi ya shilingi nusu bilioni, pesa za walipa ushuru kupitia gharama za chaguzi ndogo.
Hatua hii imezua kesi mahakamani inayotaka uteuzi huo kutangazwa kuwa kinyume cha Katiba.
Matumizi haya ya pesa yanayoepukika yamekuwa suala la kisheria, ambapo mpigakura mmoja anataka mahakama imzuie Rais Ruto kufanya uteuzi zaidi kutoka kwa Bunge ya Kitaifa na Seneti akisema unasababisha mzigo mkubwa kwa umma.
Katika juhudi za kuwazawidi wafuasi wake waaminifu kwa kuwateua kushikilia nafasi za uwaziri na kuimarisha serikali akilenga uthabiti wa kisiasa, Rais Ruto amekuwa akiwateua viongozi waliochaguliwa kuhudumu bungeni.
Kwa Rais, hatua hiyo huongeza hadhi ya Baraza la Mawaziri na kumpa umaarufu kwa faida ya kisiasa.
Lakini kwa wapigakura na walipa ushuru, hatua hizo huwalazimisha kurudi kupiga kura, ikimaanisha gharama zaidi na kupoteza muda.
Hii ndiyo sababu wakili Lempaa Suyianka, kama mpigakura, kupitia kampuni ya Mugeria, Lempaa & Kariuki Advocates, ameenda katika Mahakama Kuu akiomba uteuzi wa wabunge kuwa mawaziri utangazwe kuwa kinyume na Katiba.
Kesi yake inaangazia takwimu mpya za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwamba chaguzi ndogo nne za 2022 ziliigharimu nchi karibu nusu bilioni.
Katika Bungoma, uchaguzi ulirudiwa baada ya Seneta Moses Wetang’ula kuteuliwa na chama cha UDA kuwa Spika wa Bunge la Taifana uchaguzi huo ukagharimu Sh233,153,272.
Katika Elgeyo Marakwet, IEBC ilitumia Sh143,977,287 kufuatia uteuzi wa Seneta Kipchumba Murkomen kuwa Waziri wa Barabara na Uchukuzi.
Uteuzi wa Aden Duale na Alice Wahome ulipelekea chaguzi ndogo Kandara na Garissa Mjini zilizogharimu Sh49 milioni na Sh44 milioni mtawalia.
Uchaguzi mwingine Ugunja na Mbeere North, kufuatia uteuzi wa Opiyo Wandayi na Geoffrey Ruku kwenye Baraza la Mawaziri, unakadiriwa kugharimu Sh100 milioni.
IEBC imesema uchaguzi wa Ugunja pekee unahitaji Sh54.3 milioni.
Katika ombi lake, wakili Suyianka anasema hakukuwa na ushirikishaji wa umma kabla ya Rais kuwateua wabunge wao kuwa mawaziri, hivyo kukiuka haki yao ya kidemokrasia.
Anataka mahakama itangaze kuwa uteuzi huo unakiuka Ibara ya 201 ya Katiba inayotaka matumizi bora ya fedha za umma, pamoja na Ibara ya 10 kuhusu maadili ya kitaifa.
Anataka pia mahakama itoe amri ya kudumu ya kumzuia Rais kuwateua tena wabunge wanaohudumu kuwa mawaziri.Kenya bado inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zilizo na gharama kubwa zaidi za uchaguzi duniani.
Uchaguzi mdogo wa Novemba 27 katika maeneo 24 unakadiriwa kugharimu Sh1 bilioni. IEBC pia imekadiria kuwa uchaguzi mkuu wa 2027 utahitaji Sh61 bilioni.
Katika ripoti zake, IEBC hutaja gharama za teknolojia, idadi kubwa ya vituo vya kupigia kura, usafiri, usalama na malipo ya maafisa wa muda kama vipengele vinavyoongeza gharama.
Uchaguzi wa Kenya unagharimu mara mbili zaidi ya wastani wa kimataifa. Mwaka 2022, IEBC ilitumia Sh44.18 bilioni, sawa na Sh2,200 kwa mpiga kura, ikilinganishwa na wastani wa kimataifa wa Sh646.
Chaguzi ndogo za Novemba zitajumuisha maeneo kama Ugunja, Mbeere Kaskazini, Banissa, Kasipul, Magarini, Malava na kiti cha Seneti cha Baringo, ambacho kiliachwa wazi kufuatia kifo cha Seneta William Cheptumo mnamo Februari 16, 2025.
Banissa iliachwa wazi kufuatia kifo cha Mbunge Hassan Kullow, Magarini kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu kubatilisha ushindi wa Harrison Kombe, na Malava kufuatia kifo cha Mbunge Malulu Injendi mnamo Februari 17, 2025.