Joho: Kuunga mkono Ruto ni mkakati wa kuwa rais baadaye
WAZIRI wa Madini na Uchumi wa Baharini, Bw Hassan Joho, ameeleza sababu yake kuendelea kumuunga mkono Rais William Ruto, wakati kuna msukosuko katika Chama cha ODM kuhusu suala hilo.
Akizungumza katika eneobunge la Magarini wakati wa kampeni za mgombea wa chama hicho, Bw Harrison Kombe, waziri huyo alidokeza uwezekano wa kutafuta uungwaji mkono wa Rais katika miaka ya usoni.
Bw Joho alisema azma yake ya kuwania urais 2032 bado ipo na anaamini njia mwafaka itakuwa ni kupitia kusimama na Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027.
“Mpaka lini mtakuwa wafuasi? Hamtaki siku moja ninyi pia mfuatwe? Hamtaki kuwa na viongozi ambao wengine watawafuata?” aliuliza.
Bw Joho alisisitiza kuwa, Pwani imekuwa nguzo muhimu ya ODM kwa miongo miwili na haitakiwi kudanganywa na makundi ya kisiasa “yasiyo na mwelekeo”.
Alieleza kuwa, baada ya miaka mingi ya kumuunga mkono marehemu Raila Odinga, sasa ni wakati wa ukanda wa Pwani kutambuliwa na ‘kulipwa’ kwa uaminifu wake.
“Tumeikuwa ODM kwa miaka 20. Kama si Pwani, je, ODM ingekuwepo? Nani amelibeba chama hiki zaidi ya watu wa Pwani?” alihoji.
Joho alisisitiza kuwa kumuunga mkono Rais Ruto ni mkakati wa kisiasa unaolenga manufaa ya baadaye.
“Tumemuunga mkono Rais Ruto, na siku moja tutawaambia watu wake kuwa tulimsaidia, sasa nao watusaidie. Tuliwapa mkono, nao waturudishie,” alisema.
Kauli zake zinajiri siku chache baada ya viongozi wa Pwani kuunga mkono azma yake na kuwataka viongozi wote kumheshimu kama sura na kiongozi halisi wa siasa za Pwani.