Wahanga wa maporomoko Chesongoch kuzikwa kaburi la pamoja
KWA familia za wahanga wa maporomoko ya ardhi ya Chesongoch, Kaunti ya Elgeyo Marakwet, majonzi yao ni zaidi ya kuwapoteza wapendwa wao, sasa wanakabiliwa na swali gumu: watawazika wapi wakati mashamba, makazi na hata maeneo ya makaburi yalisombwa na maporomoko ya mawe na tope.
Kwa kuwa mashamba na makazi yaliharibiwa kabisa, familia nyingi hazikuwa na chaguo ila kukubali mazishi ya pamoja ili kuhakikisha wapendwa wao wanapumzishwa kwa heshima.
Ibada ya wafu ya zaidi ya watu 31 waliopoteza maisha katika mkasa wa Oktoba 31 huko Kerio Valley itafanyika kesho katika Kanisa Katoliki la St Benedict Christ the King, Chesongoch.
Mkasa huo uliokumba vijiji vya Kasegei, Kwenoi, Kaptul na Kipkirwon uliwaua zaidi ya watu 39 na tisa hawajapatikana, 32 walijeruhiwa na familia zaidi ya 600 kufurushwa makwao. Ni watu wanne pekee ambao watazikwa Endo na Lower Sambirir ambako familia zao zina mashamba; waliobaki watapumzishwa kwenye kaburi la pamoja karibu na kanisa.
Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Majanga wa kaunti hiyo, Bw Lawrence Mutwol, alisema kutakuwa na misa ya wafu kabla ya mazishi katika eneo lililotambuliwa. “Familia zote zimekubali kaburi la pamoja. Nyumba na mashamba yao yalisombwa na mafuriko, hivyo haikuwa rahisi kupata ardhi ya kuwazika,” alisema.
Serikali itagharamia mazishi, na alama za ukumbusho zitawekwa kwenye eneo la kaburi la pamoja. Watu tisa bado wanatafutwa, na wakipatikana pia watazikwa kwenye eneo hilo.
John Kurha wa kijiji cha Kwenoi aliyepoteza jamaa tisa alisema mazishi ya pamoja yamewapunguzia mzigo mkubwa. “Tumekubaliana kuwazika pamoja. Familia nyingi hazina mahali pa kuzika baada ya hasara hii,” alisema.
Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya eneo la North Rift linaendelea kusaidia kwa ushauri, chakula na bidhaa nyingine. Mkuu wa eneo hilo, Oscar Okumu, alisema zaidi ya watu 850 wanahifadhiwa katika kambi iliyoko Shule ya Msingi Chesongoch, huku watoto, wajawazito na wazee wakikabiliwa na utapiamlo na uhaba wa dawa.
Gavana Wisley Rotich alisema fedha zilizochangwa jijini Nairobi pamoja na msaada wa serikali zitasaidia familia kujenga upya maisha yao. Akaunti maalumu imefunguliwa kwa michango hiyo.
Bw Mutwol alitoa wito wa kuhamishwa kwa familia hizo kutoka maeneo hatari. “Haiwezekani waendelee kuishi maeneo yanayokumbwa na maporomoko. Lazima kuwe na mpango wa makazi ya kudumu,” alisema.
Viongozi wa dini pia wamejitokeza kusaidia manusura. Mchungaji Reagan Akaliche wa Kanisa la Parklands Baptist alisema msaada wa kiroho na vifaa unapaswa kuendelea hata baada ya mazishi.