Habari

Msoto jijini: Sakaja aomba idhini akope pesa za kulipa wafanyakazi mishahara yao

Na KEVIN CHERUIYOT November 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi imetangaza mpango wa kutafuta mkopo wa muda mfupi ili kukabiliana na tatizo la kuchelewa kulipa mishahara ya wafanyakazi wake.

Wakati wa kikao cha Bunge la Kaunti Novemba 19, 2025, serikali iliwasilisha hoja maalumu ikitaka idhini ya madiwani kuruhusu Kaunti kukopa fedha.

Kwa mujibu wa hoja hiyo, Gavana Johnson Sakaja anahitaji fedha hizo kulipa mishahara ya wafanyakazi wa kaunti.

“Kulingana na Kipengele cha 142 cha Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma ya 2012, naomba kuwasilisha karatasi ifuatayo katika Bunge hili: Ombi la idhini ya Kaunti ya Nairobi kukopa mkopo wa muda mfupi ili kulipa mishahara na matumizi yanayohusiana na mishahara,” ilisema taarifa ya Kiongozi wa Wengi, Peter Imwatok, iliyowasilishwa kwa niaba yake na Kiongozi wa Wachache Anthony Karanja.

Hata hivyo, madiwani walikosoa hoja hiyo wakisema haikuweka bayana masuala muhimu kama kiasi cha fedha kinachohitajika, muda wa kurejesha mkopo na benki ambayo kaunti inapanga kukopa.

Hatua hiyo inajiri wakati chama cha  wafanyakazi wa Serikali za Kaunti kinaendelea kulalamikia ucheleweshaji wa mishahara na makato ya kisheria, hali kinachosema imewasababishia mateso makubwa.

Ingawa kaunti imefuata masharti ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma ambayo inaruhusu ukopaji kwa idhini kupitia waziri wa fedha wa kaunti, madiwani waliuliza ni kwa nini Gavana Sakaja hakutoa maelezo kuhusu kiwango kamili cha mkopo anaotaka.

“Msitafute lawama. Ni ombi la idhini tu. Karatasi zimewasilishwa na sasa zitapelekwa kwa Kamati ya Bajeti na Utekelezaji ili kutoa ripoti. Tunatarajia uchambuzi wa kina,” Spika Kennedy Ng’ondi aliwaeleza madiwani.

MCA wa Ngara, Chege Mwaura, alisema kaunti ilikuwa ikijaribu kutumia vibaya mamlaka ya Bunge kwa kuwasilisha taarifa isiyo na maelezo muhimu.

“Hatuna maelezo kamili. Tunapitisha nini hasa?” alihoji Mwaura.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Wachache Karanja alimuomba Spika kulinda bunge dhidi ya kuwasilishwa kwa hoja zisizo na msingi.

“Nakuomba ulinde Bunge hili dhidi ya karatasi zisizo na thamani. Lazima waziri wa fedha  aweke viambatisho vya kutosha kabla ya kuleta hoja,” alisema.

Spika Ng’ondi alisema madiwani ndio wataamua kumpa au kumnyima gavana idhini hiyo baada ya maswali yote kufafanuliwa.

Haya yanajiri huku kaunti ikikabiliwa na ucheleweshaji wa mishahara, ambapo mishahara ya Oktoba ilicheleweshwa hadi Novemba 18, kinyume na ahadi ya Gavana Sakaja kwamba hakuna mfanyakazi angecheleweshewa malipo chini ya uongozi wake.