Gachagua: Upinzani karibu kupata mwaniaji wa urais
VIONGOZI wa upinzani jana walitangaza kuwa wapo karibu kuafikia makubaliano ya kumteua mwaniaji mmoja wa urais atakayepambana na Rais William Ruto mnamo 2027.
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, Kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa na Naibu Kiongozi wa Jubilee Dkt Fred Matiangí walionya serikali kuwa hawatakubali ufisadi, utekaji nyara na mauaji ya kiholela kuendelea nchini.
Walikuwa wakiongea katika makazi ya Bw Gachagua ya Wamunyoro, Kaunti ya Nyeri ambako mkewe Dorcas Rigathi alikuwa akitawazwa kama kasisi kutoka kwa wadhifa wa upasta ambao amekuwa akiutimikia. “Furaha yangu ni kuwatangazia kuwa mmoja aliyeketi kati yetu hapa atakuwa rais wa Kenya kati ya 2027-2032. Nitarejea kwenu hivi karibuni kuwapa habari hizi nzuri kwa sababu tuko karibu sana kukubaliana,” akasema Bw Gachagua.
Aliongeza kuwa matokeo ya uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini yatakuwa ya kwanza kudhihirisha kuwa Rais Ruto atashindwa 2027.
“Wana mwaniaji wao na sisi upinzani tuna mgombeaji wetu. Kuanzia Jumapili nitakita kambi Mbeere Kaskazini kuhakikisha tunawashinda Novemba 27,” akaongeza Bw Gachagua.
Dkt Matiangí naye alishangaa jinsi ambavyo utawala wa sasa unapuuza jukumu la kanisa na viongozi wa dini akisema hilo linaonyesha taifa linaelekea pabaya.