Uhasama upinzani Malala akidai Natembeya ni fuko
UHASAMA wa ndani kwa ndani huenda utagharimu upinzani katika chaguzi ndogo za Malava na wadi ya Kisa Mashariki kwenye Kaunti ya Kakamega ambazo zitafanyika Novemba 27.
Kuna mvutano mkubwa kati ya DAP-Kenya na DCP hasa kuhusu kiti cha udiwani cha Kisa Mashariki ambacho kina ushindani mkali.
Mnamo Ijumaa Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na Naibu Kiongozi wa DCP Cleophas Malala walikashifiana vikali na kuhusu ni chama kipi kinastahili kuwa na mwaniaji Kisa Masharaki.
Kuna dhana inayoendelea katika upinzani kuwa Bw Natembeya ni fuko wa serikali na anatumiwa kusambaratisha upinzani. Gavana huyo amekuwa akiandaa mikutano yake kivyake Malava na Kisa Mashariki huku akiwa amevalia mavazi yenye vuguvugu la Tawe.
“Huu ndio wakati wa kuonyesha kuwa jamii ya Waluhya ina hadhi. Kumpigia kura mwaniaji wa DAP-K ni kumpigia Mluhya kura,” akasema Bw Natembeya.
Alikuwa akiongea katika Wadi ya Kisa ambapo alikuwa wakati wa kumfanyia kampeni kali Abraham Ayaya. Bw Natembeya alikuwa ameandamana na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale ambaye alichaguliwa kupitia UDA lakini sasa anarindima ngoma ya upinzani.
Bw Malala alimshutumu Bw Natembeya akidai anatumiwa na serikali kusambaratisha upinzani. Pia kuna damu mbaya kati ya gavana huyo na Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa na kila mmoja amekuwa akiendesha kampeni kivyake eneobunge la Malava.
“Sote tukiwa upinzani tulikutana na Nairobi na kukubali kugawana viti kwenye chaguzi ndogo zinazokuja. Katika baadhi ya maeneo Wiper iliachia DCP, DP na Jubilee na katika maeneo mengine DCP iliachia Wiper, DAP-K na vyama vingine,” akasema Bw Malala.
Alisema kuwa katika Kaunti ya Kakamega, DAP-K na DCP zilikubaliana kuachiana vita vya Malava na Kisa Mashariki mtawalia.
“Kule Malava, DCP iliachia DAP-K nafasi ya ubunge. DAP-K iliachia DCP kiti cha Kisa Mashariki na inashangaza sasa DAP-K sasa imegeuka na ina mwaniaji Kisa Mashariki,” akasema Bw Malala.
Alitaka upinzani umakinikie kumshinda Rais William Ruto mnamo 2027 badala ya kuzua mgawanyiko na kupoteza mwelekeo.
“Adui wetu ni Rais Ruto na ni vibaya kwa viongozi kusambaratisha jahazi yetu ndani kwa ndani ilhali tuna adui mmoja,” akasema Bw Malala.
Katika eneobunge la Malava, mwaniaji wa DAP-K anakabiliwa na ushindani mkali na yule wa UDA David Ndakwa na vigogo wa serikali wanatarajiwa kukita kambi Malava kumpigie debe.