Habari

Wandayi arai wakazi na viongozi wa Nyanza kusalia katika serikali

Na DOMNIC OMBOK November 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Kawi, Opiyo Wandayi, amewataka wakazi wa Nyanza wasalie imara nyuma ya Rais William Ruto, akisema kuwa hiyo ndiyo ilikuwa nia na matamanio ya Kinara wa ODM, marehemu Raila Odinga.

Akizungumza Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Monica Kisumu, Bw Wandayi alisema kuwa uchaguzi mkuu wa 2027 unakaribia na viongozi wa Nyanza lazima waongoze raia kufanya maamuzi kwa wakati badala ya kusubiri hadi kura hiyo.
“Wakati ambapo Raila alikuwa akiondoka, alituacha tukifanya kazi kwa karibu na Rais William Ruto. Alifahamu tunakoelekea kama jamii ndiposa akatuacha serikalini,” akasema Bw Wandayi.
“Huo ni uamuzi wa busara tena wa hekima ambao aliufanya akiwa hai. Ili kumuenzi, hatufai kuondoka serikalini,” akasema Bw Wandayi huku akisisitiza ODM lazima iwe serikalini 2027.
Waziri huyo alisema kuwa Raila alikuwa amewashauri viongozi wa Nyanza washirikiane na Ruto katika siku za mwisho za uhai wake.
Ili kuenzi sifa zake za uongozi, lazima kuwe na umoja badala ya viongozi kutofautiana kuhusu mwelekeo ambao eneo hilo linastahili kuchukua.
“Baba alituonyesha njia ya kufuata kabla ya kufa. Alituambia viongozi wa Nyanza kuwa tufanye kazi pamoja na Rais,” akasema Bw Wandayi.
Waziri huyo alisema kwa sasa kuna mirengo miwili tu ya kisiasa nchini ambayo ni Serikali Jumuishi na mwingine ni upinzani.
Kwa hivyo, eneo la Nyanza linafaa kufanya maamuzi mapema kuhusu mwegemeo wake kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
“Iwapo unataka kumjua rafiki yako, basi fahamu aliyesimama na wewe wakati ambapo ulikuwa ukimhitaji. Raila alipowania urais 2007, Rais Ruto alisimama naye katika hali zote.”
“Wafuasi wake walimfanya Raila akawa waziri mkuu na hata kwenye mauti, Ruto alimpa Raila mazishi ya kitaifa. Hatuwezi kusahau hilo,” akasema Bw Wandayi.
Bw Wandayi ambaye alikuwa akihudumu kama kiongozi wa wachache bungeni, aliwaonya viongozi dhidi ya kuleta mgawanyiko Nyanza na kuwataka wale ambao wanaegemea upinzani kusema tu hadharani.
“Msiwachanganye raia, na kama unataka kujiunga na upinzani, tangaza hadharani na uende huko. Hata hivyo, hatuwezi kuruhusu mtu yeyote atugawanye, lazima kura zetu zielekee kapu moja,” akasema.
Mbunge wa Kisumu ya Kati, Joshua Oron ‘Wuon Dola’, aliunga mkono matamshi ya Bw Wandayi akisema Raila aliacha jamii ya Waluo chini ya uongozi wa Rais Ruto.
“Baba alituacha mikononi mwa Rais Ruto na kaimu kiongozi wetu Dkt Oburu Oginga hajasema vinginevyo. Umoja ni nguvu na nawaomba viongozi wenzangu tumtii Dkt Oburu,” akasema.
Hata hivyo, Naibu Gavana wa Kisumu, Mathews Owili, alitetea ODM akisema kuwa lazima kuwe na uaminifu na pia chama lazima kiwe na nguvu ndipo kitaheshimiwa.
“Kama wanachama wa ODM, tuko nyuma ya kiongozi wetu wa chama. Kama ODM ni imara, tutahakikisha tunagawana mamlaka vizuri kwenye muungano ambao tutauegemea,” akasema Dkt Owili.
Mbunge wa Mathare Anthony Oluoch aliwauliza wanasiasa ambao wanasema ODM waambie wananchi waende wapi akisema Rais Ruto ndiye ana mustakabali wa jamii ya Waluo.
“Nashangaa tumekuwa kwa Serikali Jumuishi kwa mwaka moja na miezi michache kisha mtu anatuambia tuende upinzani. Hiyo ni siasa gani? Unatoka aje serikali kujiunga na upinzani ambao pia wanataka kuwa serikali,” akasema Bw Oluoch.