Kenya kutengeneza mbolea Rais Ruto akizindua mradi wa Sh100b mjini Naivasha
KENYA itapunguza kiasi cha mbolea inayoagizwa nje ya nchi na kumakinikia uzalishaji unaondelezwa nchini ili kuwaokoa wakulima kutokana na bei ghali ya bidhaa hiyo.
Rais William Ruto jana alizindua mradi wa Sh100 bilioni wa utengenezaji mbolea eneo la Olkaria, Naivasha.
Mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya Kaishan kutoka China na Kampuni ya Kutengeneza Kawi ya Mvuke (KenGen).
“Kama nchi, tunatumia hela nyingi kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi. Hata hivyo, hivi karibuni tutapunguza kwa sababu tutakuwa tukizalisha mbolea yetu. Kiwanda hiki cha kutengeneza mbolea cha KenGen-Kaishan kitahakikisha kuwa tuna mbolea ya kutosha,” akasema Rais Ruto.
“Kutegemea mbolea inayoagizwa hupandisha bei na kusababisha wakulima waumie kwa sababu ya kupanda kwa bei kwenye soko la kimataifa ambalo huathirika na mambo mengi ikiwemo vita vya Urusi-Ukraine,” akaongeza Rais Ruto.
Kwa mwaka wa pili mfululizo, mbolea ambayo inaagizwa na serikali imepungua hali inayoashiria kuwa mpango wa serikali wa kutoa mbolea kwa bei nafuu kwa wakulima huenda ukaathirika.
Shirika la Kitaifa la Takwimu Nchini (KNBS) zinaonyesha kuwa Kenya iliagiza tani 443,701 za mbolea kati ya Januari na Juni 2025, kiwango ambacho kiligharimu Sh25.63 bilioni. Huu ulikuwa upungufu kutoka tani 445,857 wa thamani ya Sh27.71 bilioni kipindi hicho mwaka jana.
Ukikamilishwa, mradi huo wa Olkaria utazalisha tani 480,000 za mbolea kila mwaka. Rais alisema kiasi hicho kitasaidia kuwakinga wakulima kutoka bei zisizotabirika za mbolea katika soko la kimataifa.
“Changamoto za mbolea zimechangia kuongezeka kwa bei ya vyakula, zikapunguza uzalishaji na kupunguza mapato ya wakulima,” akasema.
Mnamo 2023, Kenya iliagiza mbolea zaidi ya tani 600,000 na tani 443,000 katikati ya mwaka 2025 kwa kima cha Sh60 bilioni.
“Kila shehena ya mbolea inayosafirishwa inanyima wakulima wetu nafasi. Shughuli ya leo itahakikisha kwamba tunazalisha mbolea yetu,” akasema kiongozi wa nchi.
Mradi huo utatumia megawati 165 ya umeme wa mvuke kubadilisha amonia ya kijani kuwa mbolea,Rais akisema ni mradi wa aina yake na wa kwanza barani Afrika.