Makala

‘TUTAM’: Ruto afichua ndoto yake mpya

Na BENSON MATHEKA November 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto ameeleza ndoto yake mpya ya kitaifa, akisisitiza mipango mikuu minne itakayochochea ukuaji wa nchi.

Mipango hiyo ni uwekezaji kwa raia kupitia elimu na ujuzi, uchumi wa viwandani, ujenzi wa mabwawa makubwa na miundombinu ya barabara, pamoja na nishati ya uhakika.

Akitoa hotuba yake ya tatu ya Hali ya Kitaifa katika kikao cha pamoja cha Bunge Novemba 20, 2025, Rais Ruto alisema kuwa ndoto hii inalenga kuweka msingi imara wa taifa lenye raia wenye ujuzi, uchumi thabiti, na miundombinu inayounganisha kila kona ya Kenya.

“Ndoto yetu ni kuona Kenya ikipanda hatua nyingine. Tunajitolea kushughulikia angalau vipaumbele vya kitaifa,” alisema.

Alisema inawezekana kubadilisha Kenya kuwa nchi yenye uchumi thabiti akisema katika miaka mitatu iliyopita, serikali yake imethibitisha mageuzi yanaweza kutekelezwa.
Ruto alibainisha kuwa raia wanapaswa kupewa kipaumbele kupitia elimu, mafunzo ya sayansi, ujasiriamali, na uvumbuzi.

“Serikali imeongeza bajeti ya elimu kutoka Sh 490 bilioni mwaka 2021 hadi zaidi ya Sh 700 bilioni mwaka huu, hatua ambayo imerahisisha ujenzi wa miundombinu ya shule, kuajiri walimu zaidi, na kuongeza ufadhili wa vyuo vya elimu ya juu,” alisema

Ili kutimiza ndoto hii, Rais alisema ameanzisha Idara ya Taifa ya Sayansi, Utafiti na Ubunifu ili kuendeleza masomo ya Sayansi, Tekinolojia, Uhandisi na Hisbati (STEM), kukuza uvumbuzi, na kuunda kikundi cha wataalamu wa juu katika uhandisi na sayansi.

Ruto alisisitiza pia umuhimu wa ufadhili wa wajasiriamali na ukuaji wa biashara za ubunifu ili kuunda kampuni mpya.

Akisema ni lazima Kenya ibadilike, Ruto alitoa ndoto yake ya kugeuza nchi kutoka inayoagiza bidhaa nyingi kuwa nchi ya kuuza bidhaa nje.

“Tunapaswa kuacha kutegemea mazao ya chakula yanayoagizwa kutoka nje, ambayo yanagharimu Sh 500 bilioni kila mwaka,” alisema na kufafanua mpango wake wa kufanya Kenya kuanza kutengeneza bidhaa za kilimo viwandani.

Kulingana na Rais kuwa na mabwawa makubwa na unyunyuzaji wa kisasa ni suluhisho la kuongeza uzalishaji wa ndani na kuuza nje.
Ruto alisema serikali inapanga kujenga angalau mabwawa 50 makubwa, mabwawa 200 ya kati na madogo kwa lengo la kuhifadhi maji na kuongeza ardhi ya kilimo chini ya unyunyuzaji hadi ekari 2.5 milioni ndani ya miaka mitano hadi saba. Mipango hii inalenga kugeuza maeneo ya ukame na nusu ukame kuwa nguzo za uzalishaji wa chakula, kuhakikisha utoshelevu wa chakula, kujenga uchumi wa vijijini, na maendeleo endelevu.

“Wizara ya Maji, Usafi wa Mazingira na Unyunyuzaji, ikishirikiana na taasisi zote husika, tayari imebaini maeneo mahsusi ambapo mabwawa haya yatajengwa. Miradi hii imeenea kote nchini, kutoka High Grand Falls, bwawa kubwa katika Mto Daua kaunti ya Mandera; bwawa la Isiolo–Barsalinga, Yatta kaunti ya Machakos, Sigly kaunti ya Garissa, Soin Koru kaunti ya Kisumu, Rumuruti kaunti ya Laikipia, Thuci katika kaunti za Embu na Tharaka-Nithi, Lowaat kaunti ya Turkana; bwawa la Muhoya katikakaunti za Nyeri na Kirinyaga, Narosura kaunti ya Narok na Arror kaunti ya Elgeyo–Marakwet,” alisema.

Katika hotuba yake jana, Rais Ruto alisema kuwa kawi ni moyo wa uchumi wa kisasa na Serikali ina mpango wa kuongeza zaidi megawati 10,000 katika miaka saba ijayo ili kuendesha viwanda, uchumi wa dijitali, na teknolojia ya kisasa.

Akisema Kenya ni kitovu cha uchukuzi Afrika Mashariki, Rais Ruto alieleza kujitolea kwa serikali yake kujenga barabara na reli za kisasa, pamoja na kuboresha bandari na viwanja vya ndege vya kitaifa nchini.

Mipango hii inajumuisha kuwela lami kilomita 28,000 za barabara na reli ya kisasa kutoka Naivasha hadi Kisumu na kisha Malaba. Miradi ya barabara itajumuisha Rironi–Naivasha–Nakuru–Mau Summit, Muthaiga–Kiambu–Ndumberi. Barabara nyingine ni Muthaiga–Kiambu–Ndumberi; Machakos Junction–Mariakani, MauSummit–Kericho–Kisumu; Kisumu–Busia; Mau Summit–Eldoret–Malaba; Athi River–Namanga; Karatina–Nanyuki–Isiolo;Makutano–Embu–Meru—Maua; Mtwapa–Malindi; Mombasa-Lunga Lunga, Kericho—Kisii—Migori—Isebania, Nakuru—Nyahururu—Karatina, Kisii—Oyugis—Ahero, the NorthernBypass; James Gichuru Road, Bomas—Karen—Ngong, Bomas—Ongata Rongai—Kiserian, Ngong—Isinya; and Naivasha–Kikuyu.
Ruto alisema miradi hii yote inahitaji angalau Sh 5 trilioni.

“Ili kuepuka madeni makubwa, serikali itatumia Hazina ya Taifa ya Miundombinu na Hazina Kuu ya Utajiri wa Serikali, mapato kutoka ubinafsishaji wa mashirika ya serikali. Mfumo huu unalenga kuvutia uwekezaji wa muda mrefu, kuendeleza miundombinu bila kuongeza ushuru au madeni, na kuhakikisha vizazi vijavyo vinafaidika na rasilmali za taifa,” alisema.