Habari

Mfurushe Mchina aliyedhulumu mfanyakazi raia wa Kenya, Atwoli asema

Na CHARLES WASONGA November 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU), Francis Atwoli ameitaka serikali imfurushe raia mmoja wa China aliyenaswa kwenye kanda ya video akimdhulumu mfanyakazi Mkenya.

Kwenye video hiyo iliyosambaa mitandaoni na kuwakera Wakenya wengi, Mkenya huyo anaonekana kujikinga huku Mchina huyo akimpiga teke na kuzaba makofi.

Kwenye barua aliyomwandikia Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen, Jumamosi, Novemba 15, 2025, Bw Atwoli anasema kuwa Mchina huyo ni maneja katika kampuni ya kutengeneza mabati kwa jina TCM Mabati Ltd, iliyoko mjini Eldoret, kaunti ya Uasin Gishu na mfanyakazi huyo ni mdogo wake kazini.

“Kitendo hicho ni ukiukaji wa haki na hadhi ya mfanyakazi aliyeshambuliwa. Na kama mtetezi wa wafanyakazi nchini hatutakaa tukitizama hadhi yao ikikiukwa na wageni,” Bw Atwoli akasema.

“Kwa hivyo, COTU inataka Wizara yako imfurushe  raia wa China aliyenaswa kwenye video akimdhulumu mfanyakazi Mkenya katika kiwanda cha mabati cha TCM Mabati Ltd. Bila hatua kuchukuliwa imani ya wafanyakazi nchini  kwa wizara yako na serikali kwa ujumla itakuwa imesalitiwa,” akaongeza.

Malalamishi haya ya Atwoli yamejiri wiki moja baada yake kuibua malalamishi na wito sawa hiyo wiki jana.

COTU pia ilipendekeza kufurushwa nchini kwa meneja mmoja katika Viwanda vya Kutengeneza Bidhaa za Kuuzwa Nje (EPZ) ambaye alimrushia matusi Katibu Mkuu wa Chama cha Kutetea Masilahi ya Wafanyakazi hao.

Aidha, duru zasema kuwa meneja huyo anayesimamia viwanda vya EPZ, Athi River, amekuwa akiwalazimisha wafanyakazi raia wa Kenya kuimba nyimbo za Kichina kabla, wakati na baada ya kazi.